Timu ya Kenya Harambee Stars yapata kocha mpya

Shirikisho la soka nchini Kenya limethibitisha uteuzi wa mkufunzi wa Ubelgiji Paul Put kama meneja mpya wa timu ya taifa Harambee Stars.

Raia huyo wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 61 ametia saini mkataba wa miaka miwili kuifunza Harambee Stars.

Anachukua mahala pake Stanley Okumbi ambaye amekuwa katika wadhfa huo kutoka mwaka 2016.

Raia huyo wa Ubelgiji hivi karibuni alikuwa kocha wa klabu ya Algeria USM Alger, ambapo aliiongoza klabu hiyo hadi katika nusu fainali ya kombe la vilabu bingwa Afrika.

Shirikisho la soka nchini Kenya lilimzindua kocha huyo katika mkutano wake mkuu wa kila mwaka siku ya Jumamosi.

Put amewahi kuzifunza timu za taifa za Gambia na Burkina Faso.

Chini ya uongozi wake Burkina Fasso ilimaliza ya pili katika kombe la bara Afrika 2013 ikipoteza kwa Nigeria katika fainali.

Put pia amewahi kuifunza timu ya taifa ya Jordan.

Kazi yake ya kwanza itakuwa kuiandaa Harambee Stars katika kombe la Cecafa ambalo litaanza nchini Kenya mnamo mwezi Disemba 3.

@moodyhamza