Mkufunzi wa Manchester City Pep Guardiola amechaguliwa kuwa mkufunzi bora

Mkufunzi wa Manchester City Pep Guardiola amechaguliwa kuwa mkufunzi bora wa mwezi katika ligi ya Uingereza kwa mara ya pili mfululizo.

Raia huyo wa Uhispania aliongeza taji lake la mwezi Oktoba kwa lile alilopata mwezi Septemba baada ya kikosi chake kinachoongoza ligi kufunga mabao 13 katika mechi tatu.

Winga wa City Leroy Sane mwenye umri wa miaka 21 alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi baada ya kufunga na kutoa usaidizi kila mechi .

Mchezaji wa Southammpton Sofiane Boufal alishinda taji la goli bora la mwezi kufuatia shambulio lake dhidi ya West Brom.

Mchezaji huyo wa Morocco mwenye umri wa miaka 24 alichukua mpira kutoka upande wa lango lake na kuwachenga wachezaji kadhaa kabla ya kupiga mkwaju katika kona moja ya goli ikiwa imesalia dakika tano , na hivyobasi kuipatia timu yake ushindi wa 1-0.

City ambao wanaongoza jedwali la ligi wakiwa na pointi nane mbele ya Manchester United wanacheza dhidi ya Leicester Jumamosi.

Mechi walizoshinda mwezi Oktoba ni ushindi wa 7-2 dhidi ya Stoke, Ushindi wa 3-0 dhidi ya Burnley na 3-2 dhidi ya West Brom

@moodyhamza