Leodegar Tenga apewa shavu CAF

RAIS wa zamani wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, ameula baada ya kupewa cheo katika moja ya Kamati za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Katika uchaguzi uliopita wa shirikisho hilo uliofanyika Machi mwaka huu, Tenga aligombea uwakilishi wa Afrika Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Kimataifa (FIFA), ambapo alishindwa baada ya kupata kura 20 kati ya 54 zilizopigwa. Uchaguzi huo ndiyo uliompa urais Ahmad, Rais wa Shirikisho la Soka Madagascar na kumuagusha Mcameroon Issa Hayatou, aliyeongoza kwa miaka 19.

Kwa mujibu wa taarifa ya CAF jana, uteuzi wa kamati mbalimbali ulifanyika mjini Bahrain kwenye kikao cha kwanza cha Shirikisho hilo chini ya rais mpya, Ahmad. Tenga ameteuliwa kuwa rais wa Kamati ya Usimamizi wa Leseni za Klabu na makamu wake ni Dany Jordaan wa Afrika Kusini. Uteuzi huo unamaanisha CAF bado inahitaji mchango wa Tenga, aliyewahi pia kuwa rais wa Baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Tenga ndiye rais wa kwanza wa TFF ilipofanya mabadiliko kutoka Chama cha soka Tanzania (FAT) mwaka 2005 ambapo aliwaangusha aliyekuwa Mwenyekiti wa FA Alhaji Muhidini Ndolanga na aliyekuwa Katibu Mkuu, Michael Wambura. Chini yake, TFF ilijijenga na kuwa taasisi imara kiasi cha kuvutia wafadhili mbalimbali.