Mrithi wa Jackson Mayanja kama kocha msaidizi Simba ni Juma

Raia huyo wa Burundi anachukua nafasi ya Jackson Mayanja ambaye ameondoka Simba ikielezwa ana matatizo ya kifamilia

 

Baada ya aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba Jackson Mayanja kujiuzulu nafasi hiyo, kocha Masudi Juma raia wa Burundi anatajwa kuziba nafasi hiyo.

Juma amepata mafanikio akiwa kama kocha na kuishawishi Simba kumsaini kuwa msaidizi wa Joseph Omog kwenye benchi la ufundi la Simba.

Msimu uliopita Juma alikuwa kocha wa Rayon Sports ya Rwanda na kuisaidia timu hiyo kutwa aubingwa ligi kuu. Badaaye akachaguliwa kuwa kocha bora wa msimu 2016/2017.

Amewahi kucheza klabu za APR, Rayon Sport, Prince Louis, Inter Star pamoja na timu ya Taifa ya Burundi ‘Intambamurugamba’.

Alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Burundi kilichoshiriki mashindano ya FIFA ya vijana (FIFA World Yourth Championship) mwaka 1995 nchini Qatar. Alicheza mechi tatu katika mashindano hayo.

Inaelezwa Juma ni kipenzi cha wachezaji kutokana na ukatibu wake na kuwafanya wachezaji marafiki zake, huwa anavaa jezi na kujumuika pamoja kwenye mazoezi na wachezaji.

Akiwa na umri wa miaka 40, kocha huyo bado ni kijana mwenye nguvu za kuweza kukimbizana na wachezaji mazoezini.

Anatarajiwa kutambulishwa rasmi leo Oktoba 19, 2017 mbele ya waandishi wa habari kwenye mkutano maalum wa Simba na vyombo vya habari makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Msimbazi, Dar es salaam.

@moodyhamza