Mwalimu Mkuu wa Lucky Vincent Afunguka Mazito Kuhusu Safari Iliyoua Wanafunzi

MWALIMU Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi ya mchepuo wa Kiingereza ya Lucky Vincent ya jijini Arusha, Loningo Vincent amesema kabla ya kuanza safari ya kwenda Karatu ambayo iliibua ajali iliyoua wanafunzi 33, walimu wawili na dereva, alitafakari kwa saa mbili waende huko au Njiro jijini humo kwa ajili ya mtihani wa kujipima.

Wanafunzi hao 33, walimu wao wawili na dereva walikufa baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Mitsubishi Rosa kupinduka na kutumbukia korongoni eneo la Mlima Rhotia Marera wilayani Karatu wakati wakienda katika mtihani wa ujirani mwema wa kujipima na wenzao wa Tumaini Junior.

Akizungumza wakati wa maziko ya mwanafunzi Irene Godson jana, Mwalimu Vincent aliomba samahani kwa wazazi na walezi kutokana na ajali iliyotokea ambayo si tu imeacha simanzi kubwa kwa familia husika, bali Taifa kwa ujumla.

Alisema kabla ya kuondoka shuleni hapo, alitafakari sana ndani ya saa mbili watoto hao waende Njiro jijini Arusha au Karatu kufanya mtihani wao wa kujipima. “Kabla ya watoto hawa kuondoka, nilitafakari saa mbili kama waende Karatu au Njiro hapa hapa mjini, lakini sikuwa najua kama wanakwenda kufa, wazazi mtusamehe maana hakuna aliyejua mbele kuna nini kitatokea,” alisema Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Lucky Vincent.

“Naomba nikabidhi kitabu hiki cha nyimbo za dini ambacho Irene alikuwa nacho kwenye begi Lake na walipopata ajali Irene alijitaja mara tatu kwa jina lake Irene, Irene, Irene. Kweli alikuwa akipenda sana dini kwa sababu pia ndani ya begi lake alikuwa na mafuta ya mzeituni yaliyowamwagikia wenzake wakati kila mmoja akiwa kwenye harakati za kujiokoa,” aliongeza mwalimu huyo.

Awali kabla ya kuanza ibada, Mwalimu Vincent alikabidhi Biblia kwa wazazi kwani Irene alikuwa ni mcha Mungu na kila mara alikuwa na Biblia yake na hata eneo la ajali, walimu waliokota biblia hiyo.

“Irene alikuwa ni mcha Mungu na sehemu aliyopata ajali alikuwa na Biblia yake na alikuwa akimtumaini mungu kwa kila jambo, hivyo kama walimu tunaikabidhi Biblia hii kwa familia yake,” alieleza mwalimu huyo.

Mamia ya watu walijitokeza nyumbani kwa wafiwa Kwamrombo Murriet kwa ajili ya kumuaga Irene ambaye mwili wake ulipowasili nyumbani kwa bibi na babu yake saa 6.15 mchana vilio, huzuni na simanzi vilitawala, huku bibi yake akilia zaidi kutokana na jinsi alivyokaa naye tangu akiwa na miaka miwili hadi juzi mauti ilipomfika.

Akiongoza Ibada ya mazishi, Mchungaji kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Asisisa Moshi kutoka Ushirika wa Olkerian alitoa pole kwa familia. Naye Askofu Solomon Masangwa wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini alitoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliokumbwa na msiba huo na kuwasihi wazazi kumwachia Mungu kwani hayo ni mapenzi yake Irene alizaliwa Mei 5, 2004, alisoma Shule ya Lucky Vincent na alipata ajali Mei 6, 2017 eneo la Rothia.

Juzi miili ya watoto hao iliagwa kwa pamoja huku mengine ikisafirishwa na mengine ikienda kuzikwa maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha, ambapo Hospitali ya Selian miili iliyobaki ikisubiri taratibu za mazishi ikiwa ni miwili ambayo ni mwili wa Iyan Tarimo na Irene Kishari.

Mjini Dodoma, Mwandishi Wetu, Maulid Ahmed anaripoti kuwa Serikali imeliagiza Jeshi la Polisi nchi nzima kuanzia sasa kukagua magari yote yanayosomeka kuwa ni ya wanafunzi. Sambamba na hilo, Polisi wamegizwa kukagua madereva wote wanaoendesha magari ya wanafunzi kuhakikisha magari hayo ni salama ili kuwalinda watoto.

Akijibu hoja za wabunge, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni alisema serikali imechukua uamuzi huo kutokana na ajali iliyotokea Arusha na kuua wanafunzi wasio na hatia.

                                     Source: Udaku