UGONJWA wa Ivan Wamtesa Zari Hassan,

KAMPALA: Habari mbaya zilizolifikia Amani zinadai kuwa, aliyekuwa mume wa staa wa Uganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, Tycoon Ivan Ssemwanga yu hoi bin taaban akisumbuliwa na maradhi ya shambulio la moyo (Coronary Artery Disease).

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya jijini Kampala, Uganda ambako ndiko maskani yake yalipo maeneo ya Munyonyo, pamoja na kwamba ana makazi Pretoria, Afrika Kusini, Ivan alionekana hadharani kwa mara ya mwisho akiwa amedhoofu na rangi ya ngozi kupauka, tofauti na alivyozoeleka kuwa na rangi nyeusi yenye mng’aro alipotinga kwenye Pati ya Blankets and Wine iliyofanyika Kampala hivi karibuni.

Chanzo kilichomshuhudia Ivan kilitonya: “Sisi wenyewe tulipomuona kwenye Blankets and Wine Party akiwa na rafiki yake, Ed Cheune, kwanza hatukumtambua, lakini tulipomuangalia vizuri ndipo tukamjua ni yeye. Ukweli tulishtuka sana na tulijua anaumwa. “Tofauti na alivyozoeleka kuwa ni mtu wa bata, lakini siku hiyo alikuwa mpole sana. Alikuwa hanywi pombe kali na za bei mbaya kama alivyozoeleka.

Badala yake alikuwa anakula samaki na kushushia na soda, tofauti na wadhifa wake unavyojulikana. Ivan linapokuja suala la starehe, huwa hana utani kwa sababu anajua kujiachia. “Nakumbuka tukio hilo lilikuwa Mei 11 (mwaka huu) na tangu siku hiyo hajawahi kurudi kwenye hali yake ya kawaida hadi tuliposikia amelazwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo,” kilikaririwa chanzo kimoja na mitandao ya Uganda.

Hata hivyo, Amani lilizungumza na mtu wa ndani ya familia ya Zari kwa Bongo ambaye alibumburua kwamba, kufuatia ishu hiyo, Zari amekuwa akiangua kilio kumlilia mumewe huku akiwataka watu kumuombea ‘eksi’ wake huyo kwa Mungu ili apone haraka.“Bi mkubwa hana raha kabisa, unaambiwa Ivan anamliza maana si unajua ni baba wa watoto wake watatu? ‘So’ na yeye kama binadamu lazima roho imuume kusikia mzazi mwenzake anaumwa,” alisema mtu huyo kwa ombi la kutotajwa gazetini.

Juzi Jumanne, Zari kupitia ukurasa wake wa Snapchat aliandika: “Siku mbili kwangu zimekuwa ngumu, nawaomba tumuombee Ivan.” Baadaye mama huyo wa watoto watano alitupia picha akiwa amekwenda kumjulia hali Ivan katika Hospitali ya Steve Biko Academic huko Pretoria, Afrika Kusini ambapo jamaa huyo alionekana kuwa katika hali mbaya kiafya. Ndugu, jamaa, marafiki na watoto wake watatu aliozaa na Zari wamekuwa wakimuombea ili kurejea katika uzima wake.

Source: Udaku