Gigy Amchefua Wema Ukumbini


Muuza nyago kwenye video za nyimbo za wasanii wa Bongo Fleva, Gift Stanford ‘Gigy Money’anadaiwa kumtia hasira na kumchefua staa wa sineza za Kibongo, Wema Isaac Sepetubaada ya kukutana ukumbini kwenye bethidei ya meneja wa wasanii wa muziki.

Ubuyu wa motomoto ulidai kuwa, baada ya kukutana, Gigy alidaiwa kucheza muziki kihasarahasara na mmoja wa ‘mazilipendwa’ wa Wema, jambo ambalo mlimbwende huyo hakupendezwa nalo.

Ishu hiyo ilichukua nafasi kwenye Ukumbi wa Hyatt Regency The Kilimanjaro Hotel uliopo Posta jijini Dar ambapo mastaa kibao walikuwa wageni waalikwa kwenye shughuli hiyo iliyotawaliwa na mavazi ya kizamani.

Kwa mujibu wa shushushu waWikienda aliyekuwa ndani ya shughuli hiyo, awali Wema alionekana mwenye bashasha tele akiwa na wapambe wake, lakini Gigy alipoanza makeke yake ndipo bibie huyo akapoa kama maji ya mtungi.

“Mwanzoni Wema hakuwa na tatizo kabisa na Gigy, lakini baada ya mwanadada huyo kwenda kucheza kihasara na zilipendwa wa Madam (Wema) hapo ndipo balaa likaibuka, akanywea na kumkata jicho la hasira, hata wale wapambe wake (Wema) wakaanza kumvimbia Gigy baada ya kuona anataka kuharibu shangwe za mama la mama.

“Gigy alionekana ni mwenye furaha tele, kwani alikuwa amepiga maji ya kutosha (pombe) hivyo hakujali hata kidogo kama anamkwaza mtu, isitoshe kilichoharibu zaidi ni baada ya jamaa kunogewa na manjonjo ya Gigy na kumzawadia wigi lake alilokuwa amevaa,” aliongeza sosi.

Baada ya kuinyaka ishu hiyo,Wikienda lilimtafuta Gigy na kumuuliza kulikoni kumkera Wema kwa kumchezea vibaya bwana wake wa zamani ambapo bila hiyana alifunguka:

“Ni kweli nilicheza na huyo mtu tena kwa kujinafasi kwa sababu ilikuwa ni sehemu ya furaha, sikuona sababu ya kujivunga eti kwa sababu nitamuudhi Wema au mtu yeyote yule.

“Kwanza yeye ameshaachana naye kitambo kama bado ana wivu naye atajijua mwenyewe,” alisema Gigy.

Jitihada za kumpata Wema hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuita bila kupokelewa na hata alipotumiwa chatting kupitia WhatsApp zilionesha kupokelewa lakini hakujibu.

Source: udaku