FAHAMU UKWELI KUHUSU BIFU YA MPOKI NA MASANJA.

Siku chache tangu m c h e k e s h a j i mwenye jina kubwa Bongo, Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ auage ukapera kufuatia ndoa yake iliyozua gumzo, nyepesi nyepesi za mjini zinasema kuwa kutoonekana katika shughuli hiyo kwa msanii mwingine, Silvery Mujuni ‘Mpoki’ kunatokana na bifu zito lililopo kati yao, Risasi Mchanganyiko limedokezwa.

Mpoki na Vengu walikuwa ndiyo wasanii pekee wa kundi mahiri la vichekesho la Orijino Komedi ambao hawakutokea katika shughuli hiyo ambayo awali ilianzia katika Kanisa la Miito ya Baraka Kariakoo na baadaye katika Ukumbi wa Prime Rose, Mbezi Beach jijini Dar. Inafahamika kuwa Vengu ana matatizo ya kiafya na hajaonekana hadharani kitambo sasa.

KISIKIE CHANZO

Chanzo chetu ambacho kiliomba hifadhi ya jina lake, kilisema ilikuwa ni jambo la lazima kwa Mpoki kuwepo katika shughuli hiyo, kwani alikuwa jijini, lakini kuwepo kwa tofauti kati yao, kulisababisha mtangazaji huyo wa redio kwa sasa, kutoonekana kwenye harusi na tafrija ya memba mwenzake huyo, anayetajwa kuwa ndiye mwenye mafanikio zaidi kuliko wote ndani ya kundi lao. “Mimi nawaambieni Masanja na Mpoki kuna kitu. Jiulizeni kwa nini waigizaji wengine wa kundi lao walijitokeza kumsapoti mwenzao kwa kukata mauno kasoro lakini Mpoki hakuhudhuria wakati alikuwa hapahapa mjini akiendelea na mishemishe zake? Fuatilieni, kuna kaukweli,” kilisema chanzo hicho.

RISASI MCHANGANYIKO LAINGIA MZIGONI

Kufuatia madai hayo, gazeti hili liliingia mzigoni kufuatilia ukweli wa jambo hilo na sehemu ya kwanza, ilikuwa ni kwenye mitandao ya kijamii ambako lilihoji kulikoni Orijino Komedi? Katika mtandao mmoja maarufu Bongo, wachangiaji mbalimbali nao walionesha kuhoji sababu za msanii huyo, ambaye pia hujiita Mwarabu wa Dubai, kutoonekana, wakidai kuwepo kwa matatizo kati yao, yanayosababishwa na masilahi. “Ishu siyo Masanja na Mpoki ni Mpoki na Kundi la Orijino Komedi. Kundi linaonekana kama limekufa, hawatoi kazi mpya, kila mtu anaonekana kufanya kazi kivyake na  hawashirikiani katika shughuli za kijamii kama zamani,” aliandika mchangiaji mmoja katika mtandao huo. Mchangiaji mwingine alisema kuwa tatizo linalotokea ni ukweli kuwa Masanja Mkandamizaji, ambaye ni kinda katika sanaa kuliko Mpoki na Joti, amefanikiwa sana kutoka kimaisha kuliko wenzake, jambo linalowafanya waingiwe na kinyongo. Baada ya mitandao hiyo na kuona maoni hayo ya wachangiaji, gazeti hili liliamua kukata mzizi wa fitina kwa kujaribu kuwafikia wasanii hao ili kupata ukweli wao.

HUYU HAPA MASANJA MKANDAMIZAJI

“Mimi na Mpoki ni kama ndugu kaka, hakuna kitu kama hicho, siku ya ndoa yangu alikuwa na mambo yake binafsi, ndiyo maana hakuweza kutokea, lakini wengine walimuwakilisha, kwa hiyo hizo tetesi hazina mashiko kabisa,” alifunguka Masanja na kuongeza; “Madai ya kundi kumomonyoka pia hayana ukweli wowote, Orijino Komedi inaendelea na kazi zake kama kawaida, napenda kuwaambia tu Watanzania kwenye kundi letu kulikuwa na mlango wa kuingilia tu na hakuna wa kutokea, kama mnabisha au mnataka kuamini zaidi basi zungumza na msemaji wa kundi, Seki,” alisema.

MPOKI ASAKWA, AKAUSHA

Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Mpoki kupitia simu yake ya mkononi, lakini haikupokelewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno, alikataa kusema lolote, badala yake akajibu; “Namba ya Masanja hiyo muulize,” alisema huku akitoa namba ya muigizaji mwenzake huyo. SEKI SASA Kiongozi na msemaji wa kundi hilo, Sekioni David maarufu kama Seki, alisema kundi lao lipo imara ingawa ni muda mrefu hawajatoa kazi. “Wasanii wapo mapumziko na tunatumia muda huu ili kuboresha mikataba yetu ili tutakaporudi, tutakuja na kitu kingine tofauti kabisa.” Kuhusu kutoonekana kwa Mpoki harusini na kwenye sherehe, msemaji huyo ambaye pia ni msanii wa kuigiza sauti za watu, alisema; “Kwa nini humuulizi Vengu, kulikuwa na wawakilishi wake pale mbona huwasemi? Si unafahamu kama Mpoki pia ni MC? Siku hiyo alikuwa na kazi nyingine ndiyo maana hakutokea.”

Habari hii imeandikwa na @Joplus_

Source: Muungwana Blog