AJALI ILIYOUA WATOTO 32: Jalada la Mmiliki wa Shule Kutua kwa DPP..!!!

MMILIKI wa Shule ya Lucky Vincent iliyokumbwa na msiba wa kuondokewa na wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wake katika ajali iliyotikisa taifa mwishoni mwa wiki, Innocent Moshi, anaendelea kushikiliwa na polisi na jalada lake litafikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ili kujua hatima yake.

Aidha, wakati Jeshi la Polisi likitoa taarifa hiyo kupitia Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuf Ilembo, suala hilo lilinguruma pia bungeni mjini Dodoma jana wakati Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alipohoji sababu za mmiliki wa shule, Mushi, kushikiliwa huku trafiki katika vizuizi vinne walioruhusu gari lililobeba wanafunzi hao wakiachwa.

Kama hiyo haitoshi, juzi, Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, ilitangaza kufanyika kwa operesheni kabambe ya kukagua uthabiti wa magari yote yanayobeba wanafunzi nchini.

Ajali hiyo iliyoshitua taifa na kuacha simanzi kubwa ilitokea Jumamosi iliyopita wakati basi lililobeba wanafunzi wa shule hiyo ya awali na msingi lilipoacha njia na kutumbukia kwenye korongo katika eneo la Rhotia Marela, Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha.

Watoto 32 waliokuwamo kwenye gari hilo lililokuwa likiwapeleka kufanya mtihani wa kujipima wa ujirani mwema katika Shule ya Msingi Tumaini walifariki dunia, pamoja na walimu wao wawili na dereva wao.

Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu aliongoza maelfu ya wananchi kuaga miili ya marehemu hao kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Jumatatu huku Jeshi la Polisi likianzisha uchunguzi mkali uliohusisha kukamatwa kwa mmiliki wa shule, Moshi.

JALADA KWA DPP
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana kuhusiana na uchunguzi wa ajali hiyo, Kamanda Ilembo, alisema bado wanaendelea na uchunguzi wao na kwamba, kazi hiyo ikikamilika watalipeleka jalada kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili mwishowe lipitiwe na DPP na kujua kama kuna hoja za kisheria kwa mmiliki wa shule hiyo (Moshi) kufikishwa mahakamani.

 Source: Udaku