Serikali imepiga marufuku kufunga ndoa bila ya cheti cha kuzaliwa

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe amepiga marufuku watu kufunga ndoa ya aina yeyote,iwe ya serikali, kimila au ya dini bila kuwa na cheti cha kuzaliwa kuanzia Mei Mosi, mwaka huu.

Amesema hayo Alhamisi hii akiwa katika ziara yake mkoani Morogoro na kuongeza kuwa serikali imeamua kufanya hivyo ili kupata takwimu sahihi za wananchi wake zitakazosaidia kupanga mipango ya kimaendeleo sanjari na kuzuia wageni kuingia kinyemela nchini.

Pamoja na mambo mengine, Dk.Mwakyembe amewataka Wakala wa Usajili wa vizazi na Vifo (RITA), kuhakikisha inasimamia sheria ya usajili ambapo amesema kuwa bila kuwa na takwimu sahihi za vizazi na vifo ama ndoa inasababisha nchi kushindwa kusonga mbele kimaendeleo.

“Wenzetu nchi zilizoendelea suala la usajili wamelipa kipaumbele lakini sisi bado tuko nyuma, kwa mfano Mkoa wa Morogoro kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, inaonyesha kuna jumla ya wakazi milioni 2.2, lakini waliosajiliwa na kuwa na vyeti vya kuzaliwa ni asilimia 11 pekee huku wengine wakiwa bado hawasajiliwa,” amesema.

                        Source: Millard ayo