Zari Adaiwa Kuwa na Roho Ngumu.


Kifo cha mama mzazi wa staa ambaye ni mjasiriamali Afrika Mashariki, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, Halima Matovu Hassan ‘Mama Zari’ (58) kilichojiri Alhamisi iliyopita nchini Uganda, kimeibua gumzo ambalo si la nchi hii.

Gumzo hilo kutoka nyumbani kwa mama Zari huko Busunju, Munyonyo jijini Kampala, Uganda lilihitimishwa wikiendi iliyopita na vyombo vya habari za mastaa nchini humo baada ya mazishi ya mama Zari yaliyofanyika mchana wa Ijumaa iliyopita, kuwa, Zari ana roho ngumu aisee!

Kwa mujibu wa vyombo hivyo, wakati wa kifo cha aliyekuwa mume wa Zari, Tycoon Ivan Ssemwanga ‘Don Ivan’ aliyefariki dunia Mei 25, mwaka huu, mwanamama huyo, kabla, wakati na baada ya mazishi ya baba watoto wake huyo alikosolewa juu ya tabia alizozionesha wakati wa msiba huo.

Ilielezwa kuwa, baadhi ya mambo aliyoyafanya wakati ule ikiwemo kuposti vitu mitandaoni, mara akikata mauno au kujiachia bwawani na mwanaume na kuibua utata, safari hii ilikuwa cha mtoto bila kujali majonzi ya kufiwa na mama yake kipenzi.

 

CHANZO CHATIRIRIKA
“Ile kali aliyoitoa kipindi kile wakati wa kifo cha Ivan ilikuwa cha motto maana angalau alionyesha kuwa amefiwa kwa kuangua kilio na kuonesha majonzi lakini safari hii, tena akiwa amefiwa na mama yake mzazi aliyemlea bila baba (single parent) ndiyo ameweka rekodi na kuonesha kweli ana roho ngumu.

“Wewe angalia hata video za tukio lenyewe (mazishi na maziko ya mama yake), Zari anaonekana mkavu kabisa, halii hata tone. Tofauti na ndugu zake kama mdogo wake (Zuleha Hassan) ambao wanaonekana wakilia hadi wengine wakizimia.

“Kibaya zaidi ni kitendo cha kugandana na huyo mpenzi wake wa sasa (msanii wa Bongo Fleva) kisha kuoneshana mahaba kwa kushikanashikana mbele za watu bila kujali yupo kwenye msiba mzito wa mama yake mzazi.

“Kama hiyo haitoshi, Zari akiwa kama dada mkubwa alitakiwa kuwaongoza wadogo zake kuomboleza kifo cha mama yao, lakini yeye ndiyo kwanza alikuwa anachati kwenye simu na kuachia tabasamu kama vile hajafiwa.

 

Akiwa Busy na Simu Msibani

“Wengine wanasema Zari anafanya mambo yake ‘Kizungu’, lakini kiukweli amewastaajibisha wengi kwa kutoonesha machungu ya kumpoteza mama yake kipenzi.

NANI ZAIDI?
“Unajua angalau kwa Ivan, Zari alionesha machungu kidogo. Sasa hapo ndipo kumeibuka mjadala kwamba inawezekana alikuwa na uchungu zaidi wa kufiwa na aliyekuwa mpenzi wake kuliko mama yake?

“Kiukweli ishu hii imewagawa watu maana kuna wanaosema machungu yanatofautiana kwani wapo wanaoumizwa zaidi na wazazi lakini pia wapo wanaoumizwa zaidi na wapenzi.

“Wapo wanaoamini kuwa inategemea tu na namna mtu alivyoshibana na huyo aliyetangulia mbele ya haki na ubaya ni kwamba hakuna kipimo au kiwango kamili cha namna mtu anavyoguswa na jambo.

“Kwa mantiki hiyo, wapo wanaoamini kuwa, inawezekana Zari alionekana hivyo kwa nje lakini si ajabu kwa ndani alikuwa anaumia kupita maelezo,” kilitiririka chanzo kilichohudhuria mazishi na maziko hayo kilichokaririwa na vyombo hivyo vya habari.

MZAZI MWENZA AMTETEA
Katika kumtetea Zari, mpenzi wake wa sasa aliyezaa naye watoto wawili, mmoja wa kiume, alipoulizwa juu ya namna mwanamama huyo anavyoonekana kutochukulia jambo hilo kwa uzito tangu mama yake huyo akiwa amelazwa ambapo alionekana akijiachia na kukata mauno kwa furaha, jamaa huyo alidai kuwa, wakati Zari anafanya hivyo yeye pamoja na ndugu zake wengine walikuwa wamepata habari kuwa, mzazi huyo aliendelea vizuri.

Jamaa huyo alipoulizwa kuwa, kwa nini hakwenda kumuona mkwewe wakati amelazwa alijitetea kuwa, siyo kila kitu cha familia cha kuwekwa wazi na kwamba watu waache kudili na familia za wengine badala yake wadili na familia zao na wawe na mipaka ya kushabikia mambo.

NENO LA MHARIRI
Zari amepitia changamoto nzito ya kufiwa na aliyekuwa mumewe aliyeishi naye yapata miaka 10 na kujaliwa watoto watatu wa kiume na sasa ameondokewa na mama yake mzazi, naye kama mwanadamu, siyo mkamilifu hivyo anahitaji faraja zaidi ya kupigwa mawe.

Pamoja na kwamba wengi wanasema kuwa, Zari ana roho ngumu lakini pia ana mazuri yake ya kuigwa kwa kuwa ni mfano wa wanawake watafutaji duniani.

Source: Udaku