walipofikia ukarabati wa pitch ya uwanja wa Taifa

Kwa takribani mwezi mmoja sasa, uwanja wa Taifa umekuwa kwenye matengenezo ya sehemu ya kuchezea. Mara ya mwisho uwanja huo umetumika kwenye mechi ya Ngao ya jamii ya watani wa jadi Simba na Yanga August 23 na kesho yake nyasi za uwanja huo zilifumuliwa na kuanza matengenezo rasmi.

Tulifeli ukaguzi

“Wakati tunafikiria kuileta Everton kulikuwa na wataalamu kutoka Uingereza ambao walikuja hapa kuangalia vitu mbalimbali kama vile usalama wa timu zao, malazi kwa maana ya hoteli, usafiri na mwisho wakasema wanataka kuona miundombinu ya kuchezea kwa maana ya uwanja kwasababu na wao wana vigezo vyao kuanzia kwenye sehemu ya kuchezea, vyumba na vyoo lazima vikidhi viwango vile ambavyo vinahitajika kimataifa.

“Tuliweza kufaulu kwa maana ya hoteli, usalama na usafiri vilevile suala la mizunguko kwasababu unajua Dar es Salaam ni moja ya sehemu zenye foleni, lakini ilipokuja kwenye uwanja hatukufaulu kwasababu uwanja ulionekana haufai

“Tulikuwepo wakati wanachimba kuangalia udongo ukoje, nyasi zikoje kama zinaweza kufaa kuchezea mpira, kwetu sisi watanzania zilikuwa zinafaa lakini kwao walikuwa wanaona hivyo.

“Wakaenda kuangalia miundo mbinu mingine kama vile vyumba vya kubadilishia nguo, vyooni na sehemu nyingine na walichukua sampuli wakaondoka nazo kwenda Uingereza kuangalia lakini kwakweli tulifeli.

Awamu ya kwanza

“Sasa kilichotokea kwa SportPesa ili kuweza kuileta Everton, ilikuwa ni lazima kutengeneza upya uwanja kwenye sehemu ya kuchezea na vyumbani. Muda ulikuwa hautoshi na wataalam wakaja kuangalia wanawezaje kuutengeneza uwanja katika hatua ya awali ili kuiwezesha Everton kuja kucheza.

“Zikatengenezwa nyasi ambazo zinaweza kuota haraka ili kwa wiki tatu au nne ziwe zimeshakamilika, lakini nyasi hizo zisingeweza kudumu, sana sana zitumike kwa miezi mitatu na baada ya hapo ije awamu ya pili ambayo itengeneze nyasi za kisasa zitakazodumu kwa kipindi kirefu hata miaka kumi ambazo hata gharama yake ni kubwa.

Gharama

“SportPesa imetumia hela nyingi sana kuweza kutengeneza ile hatua ya kwanza na hii hatua ya pili ambayo imekwangua kila kitu tukaanza upya na ukienda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwasasa ni vya kimataifa kabisa.

Hapa ndipo utakapoona kuwa sababu kubwa ya SportPesa kufanya hizo kazi si tu kwasababu ya Everton inakuja, lakini pia kuweza kutoa mchango wetu kwa taifa la Tanzania ili kuweza kuwa na miundombinu bora zaidi ambayo ina viwango vya kimataifa.

“Ukumbuke kuwa Tanzania itaandaa mashindano ya vijana ya mwaka 2019 na uwanja ule utakuja kupimwa ili kuona kama umefuzu viwango vya kimataifa. Na hali ilivyo sasa ni lazima watasema Naam! Na hiyo yote ni kwasababu ya SportPesa,”

Serikali inasemaje?

Serikali kwa upande wake imeishukuru Kampuni ya SportPesa kwa ukarabati huo huku wakisema kuwa sasa mambo yatakuwa safi kuelekea maandalizi ya fainali za vijana za AFCON za mwaka 2019 ambapo Tanzania atakuwa mwenyeji huku pia wakisisitiza kuendeleza mahusiano yao mazuri na SportPesa.

“Tunategemea kuwa na mashindano ya AFCON U-17 mwaka 2019 sasa kuna mahitaji mengi, hatusemi kuwa uwanja wetu haukuwa na mahitaji hayo, lakini kulikuwa na vitu vichache vya kurekebisha kwamfano kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kitu ambacho SportPesa pia wamekifanya, kwa hiyo uwanja unakuwa na vigezo zaidi kuandaa mashindano makubwa zaidi ya AFCON, kwahiyo marekebisho haya yana maana kubwa sana kwa sisi wizara na taifa kwa ujumla wake.

“SportPesa kwa kweli wameonesha mfano, wamejitahidi sana kudhamini vilabu mbalimbali, wametusaidia kurekebisha uwanja na kama sikosei gharama za kurekebisha uwanja zimefika takribani bilioni 1.3, ni hela nyingi sana hivyo sisi tunawashukuru na tunaendelea kuwaomba wasikate tamaa,” alisema Mh. Yusuph Singo ambaye ni Mkurugenzi wa michezo wa Wizara ya Habari, Sanaa, utamaduni na michezo.

story@moodyhamza