Mzazi kuepuka/kutupilia mbali jukumu la uzazi la kuwalea na kuwatunza watoto

Mzazi kuepuka/kutupilia mbali jukumu la uzazi la kuwalea na kuwatunza watoto ni dhambi kubwa mbele ya Allah. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Kunatosha kabisa kumpatisha mtu dhambi kwamba yeye anawatelekeza wanao mtegemea (mke, watoto na wazazi)”. Abu Daawoud & wengineo-Allah awarehemu.

 

Ni dhahiri kutokana na hadithi hii tuliyo inukuu kwamba inatosha kabisa mtu kufikwa na ghadhabu ya Allah na kupata dhambi kwa sababu ya kuwatekeleza na kutowajali wale wote wanao mtegemea kimaisha kwa mujibu wa sheria. Kunaweza kuwa na sura kadhaa za baba kuibwaga na kuitelekeza familia yake:

1)           Kutumia kwa ufakhri na sifa huku akizipuuzia haki za familia.

2)           Kutumia kwa ajili ya anasa na kushibisha matashi na tamaa za nafsi yake, huku akiiacha na njaa familia yake.

3)           Kutumia kwa kutoa sadaka na kufanya ihsani, huku akishindwa kukidhi mahitaji ya familia yake kwa sababu ya kutokujua kwake misingi ya Uislamu.

4)           Kuwatia njaa watoto kwa sababu ya uvivu na ugoigoi wake na kutokutaka kufanya kazi itakayo mpatia chumo.

Hata hivyo, vyo vyote itakavyo kuwa, malezi/matunzo ya watoto ni jukumu la kidini la kila baba. Kuzembea na kulibwaga jukumu hili ni dhambi kubwa mno.

 

  1.          Fedha/matumizi yalipayo zaidi:

Sayyidina Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-amemnukuu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema: “Iwapo utaitumia dinari yako moja katika njia ya Allah, nyingine (ukaitumia) kumuacha huru mtumwa. Nyingine (ukaitoa) kama sadaka kwa masikini na moja kwa ajili ya familia yako. Kati ya dinari zote hizi nne, yenye ujira  mkubwa kuliko zote ni ile uliyo itumia kwa ajili ya familia yako”. [SAHIH MUSLIM]. Hili linaelezwa kwa uwazi na hadithi ifuatayo inayo simuliwa na Sayyidina Thaubaan-Allah amuwiye radhi-akisema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Dinari yenye baraka ni ile inayo tumiwa kwa ajili ya familia ya mtu, inayo tumiwa katika (jihadi) njia ya Allah na ile inayo tumiwa kwa ajili ya wale walioko katika njia ya Allah”.

Abu Qulaabah – mmojawapo wa wapokezi wa hadithi – anasema kwamba Mtume wa Allah alianza kuzungumzia suala la mtu kutumia kwa ajili ya familia yake, kisha akasema: “Nani anaweza kustahiki zaidi kuzawadiwa thawabu na Allah kuliko yule mtu anaye tumia kwa ajili ya watoto wake ili kuwakinga na kuomba na kuwa na maisha mazuri!” Tirmidhiy-Allah amrehemu.

 

  1.            Baba mwenye kheri/bahati zaidi:

Sayyidina Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-anahadithia kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Mtu anaye chuma kwa njia za halali kwa ajili ya kujiokoa na uombaji na kupata riziki ya familia yake na kumsaidia jirani yake. (Mtu huyo) siku ya Kiyama atakutana na Allah Taala akiwa na uso ung’arao mithili ya mwezi angavu. Na yule anaye chuma kwa njia za haramu kwa lengo la kuwa na hali nzuri zaidi na kuonyesha uwezo wake wa kifedha kwa wengine. (Huyo) atakutana na Allah (huku Allah) akiwa na hasira kuu (juu yake)”. Al-Baihaqiy-Allah amrehemu.

 

  1.          Mama atumiaye mali kwa ajili ya wanawe:

Uislamu haukuwatwika akina mama mzigo wa kuchuma kwa ajili ya familia zao. Dhima hii wamepewa akina baba peke yao, wao ndio wana jukumu la kuikimu familia kimaisha. Mgawanyo huu wa majukumu wa baba na mama ni muhimu mno katika wigo huu wa familia na malezi ya watoto kwa ujumla. Mgawanyo huu ndio unao leta kani kwa kila mmoja wao kujitahidi kwa kadri ya uwezo wake kutimiza majukumu na wajibu wake kuielekea familia yake. Lakini mgawanyo huu haumaanishi kwamba mama mwenye uwezo, akiutumia uwezo wake huo kuwahudumia watoto wake hatalipwa ujira na Allah Taala. Katika hali/mazingira ambamo waume wamekufa na kuwaacha wajane na watoto au waume hao wana kipato duni kisicho weza kukidhi mahitaji ya familia. Wanawake wanao chuma na kutumia chumo na pato lao hilo katika kuikimu familia, watalipwa ujira maridhawa na Allah Taala. Sayyidatna Ummu Salamah-Allah amuwiye radhi-anahadithia kwamba siku moja alimuuliza Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Je, mimi nitalipwa (na Allah Taala) kwa kutumia kwa ajili ya watoto wa Abu Salamah (marehemu mume wangu)? Siwezi kuwaacha katika uhitaji na njaa wakizunguka  kama omba omba mlango hadi mlango. Na zaidi ya yote hayo, wao ni wanangu (pia, kwani mimi ndiye mama yao)”. Mtume wa Allah akamjibu: “Naam, hapana shaka kuwa utalipwa na Allah Taala kwa cho chote utakacho kitumia kwa ajili yao”. [RIYAADHUS-SWAALIHEEN]

Mama wa waumini; mke wa Mtume wa Allah, Ummu Salamah-Allah amuwiye radhi-alikuwa na watoto wawili wa kiume na wawili wa kike kwa mume wake wa kwanza; Abu Salamah. Swali hilo alilo uliza lilikuwa linawakhusu watoto hawa. Hadithi hii inatuwekea wazi mambo mawili:

MOSI: Ingawa kisheria mama hawajibishwi kuwakimu watoto kimaisha, lakini akifanya hivyo atalipwa ujira na Allah Taala.

PILI: Inatuonyesha mtazamo anao paswa kuwa nao mama muumini kuwaelekea wanawe. Sayyidatna Ummu Salamah alihisi kuwajibika kwa wanawe baada ya kifo cha baba yao kutokana na upendo na huruma aliyo kuwa nayo juu yao. Na aliona kuwa huo ni wajibu wake na kutaka uma ulitambue hilo pale alipokwenda kumuuliza Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na kusema: “…Siwezi kuwaacha katika uhitaji na njaa wakizunguka  kama omba omba mlango hadi mlango”. Na wakati huo huo akiwa na shauku na duku duku la kutaka kujua  iwapo atapata ujira na thawabu akhera kwa Allah Taala kutokana na tendo lake hilo. Hili iwapo linaashiria jambo, basi jambo hilo halitakuwa jingine zaidi ya kwamba daima muislamu huyafikiria maisha ya baada ya kufa. Na fikra hizi ndizo zimtiazo nguvu na mori wa kutenda amali njema ili akapate jazaa nono mbele ya Allah Taala kesho akhera.

@moodyhamza

Facebook Notice for EU! You need to login to view and post FB Comments!