SWALA YA KUOMBA MVUA

Hii ni swala iliyopitishwa na kuwekwa na sheria wakati mvua ifungikapo au kukauka chem chem (vyanzo vya maji). Na swala hii imesuniwa wakati itakapodhihiri sababu pelekeshi yake na itafutu kwa kuondoka sababu pelekeshi hiyo kama vile kuanza kunyeesha kwa mvua kabla ya kuanza kuswali.

  1. Namna ya kuswali:

Swala ya kuomba mvua ina namna tatu katika kuswaliwa kwake:-

  1. a) Namna ya chini: Kuleta dua ya kuomba mvua wakati wo wote aupendao.
  2. b) Namna ya kati: Hii ni kuleta dua ya kuomba mvua baada ya rukuu ya rakaa ya mwisho ya swala tano za fardhi na baada ya kutoa salamu.
  3. c) Namna kamilifu: Hii ndio namna inayobainishwa katika somo hili kama ifuatavyo:-

 

MOSI:

Imamu au naibu wake atawaamrisha watu kutenda mambo yafuatayo:-

  1. Kuleta toba ya kweli.
  2. Kutoa sadaka kwa mafakiri.
  3. Kujitoa katika jarima ya dhulma kwa kurejesha walivyodhulumu kwa wadhulumiwa.
  4. Kusafi nia baina yao, na
  5. Kufunga siku nne mfululizo.

Yamependekezwa mambo haya kutokana na nguvu ya athari yake katika suala zima la kupokelewa na kujibiwa dua, kama lilivyothibiti hilo katika hadithi nyingi sahihi.

 

PILI:

Imamu atatoka nao katika siku ya nne ya swaumu yao hiyo wakiwa wamevaa nguo chakavu, wakifunikwa na unyenyekevu na utulivu wa hali ya juu kabisa. Awaongoze mpaka mawandani (mahala pa wazi mbali na makazi yao), hapo atawaswalisha rakaa mbili mithili ya zile rakaa mbili za swala ya Idi. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alitoka akiwa mnyenyekevu amevaa nguo chakavu akionyesha udhalili wa haja, akaswali rakaa mbili kama anavyoswali katika swala ya Idi”. Ibn Maajah (1266) & wengineo-Allah awarehemu.

 

TATU:

Wakimaliza kuswali, Imamu atawakhutubia khutba mbili mithili ya zile khutba za swala ya Idi. Ila tu badala ya kuzifungua kwa takbira kama ilivyo katika swala ya Idi, atazifungua kwa kuleta Istighfari tisa mwanzoni mwa khutba ya kwanza na saba mwanzoni mwa ile ya pili. Hili ni kwa mujibu wa kauli tukufu ya Allah: “…OMBENI MAGHUFIRA (msamaha) KWA MOLA WENU. HAKIKA YEYE NI MWINGI WA MSAMAHA. ATAKULETEENI MAWINGU YANYESHAYO MVUA NYINGI. NA ATAKUPENI MALI NA WATOTO NA ATAKUPENI MABUSTANI NA ATAKUFANYIENI MITO”. [71:10-12]

Akishaianza khutbah ya pili na kufikia kiasi cha theluthi yake, khatibu ataelekea Qiblah akiwapa mgongo maamuma wake. Ataigeuza shuka yake (nguo ya kujitanda juu) kwa kuifanya juu chini, chini juu, kulia kushoto na kushoto kulia. Atafanya hivyo kwa ajili ya kuzidi kuonyesha udhalili na uhitaji kwa Allah Mshindi Mtukuka. Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-amesema: Siku moja Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alitoka kwenda kuomba mvua. Akatuswalisha rakaa mbili bila ya adhana wala iqaamah, kisha akatukhutubia na kumuomba Allah, akaugeuzia uso wake upande wa Qiblah ilhali ameinyanyua mikono yake. Halafu akaigeuza shuka yake (ya kujitanda), akauweka upande wa kulia kushoto na ule wa kushoto kulia”. Ibn Maajah (1268)-Allah amrehemu.

Na ni suna watu wafanye mithili ya afanyavyo Imamu wao. Na pia ni suna khatibu kukithirisha kuleta Istighfari, dua, toba, kunyenyekea na kutawasali na watu wema wacha-Mungu. Imepokelewa kutoka kwa Anas-Allah amuwiye radhi: Kwamba Umar Ibn Al-khatwab-Allah amuwiye radhi-watu wanapopatwa na ukame alikuwa akiomba mvua kwa jaha ya Al-Abas Ibn Abdil-Mutwalib, akisema: Ewe Mola wa haki wee! Hakika sisi tulikuwa tunatawasali kwako kwa jaha ya Mtume wetu nawe ukitunywesheleza. Na kwa hakika sisi (hivi sasa) tunatawasali kwako kwa jaha ya ami wa Mtume wako, basi tunakuomba utunywesheleze. Akasema: Basi hunyweshelezwa (hushushiwa mvua)”. Bukhaariy (964)-Allah amrehemu.

 

NNE:

Ni suna wawatoe na kwenda nao mahala pa kuswalia watoto wadogo, wazee, vikongwe na wanyama, kwa sababu janga hili liwapatalo ambalo wanatoka kwa ajili yake linawakumba wote pamoja. Na wala haitakikani kuwazuilia Ahlu-dhimah (Dhimiyuuna) kuhudhuria ibada hii ya kuomba mvua.

 

III.          Baadhi ya dua zilizopokewa katika swala hii:

“ALLAAHUMMAJ-‘ALHAA SUQYAA RAHMAH, WALAA TAJ-‘ALHAA SUQYAA ‘ADHAAB, WALAA MAHQI WALAA BALAA, WALAA HADMI WALAA GHARAQ. ALLAAHUMMA ‘ALAAD-DHWIRAABI WAL-AAKAAMI, WAMANAABITIS-SHA’ARI WABUTWUUNIL-AUDIYAH, ALLAAHUMMA HAWAALAYNAA WALAA ‘ALAYNAA. ALLAAHUMMAS-QINAA GHAYTHAN MUGHIYTHA, HANIY-AN MARIY-‘AN, SAHAN ‘AAMAN GHADAQAN TWABAQAN MUJALLALA, DAAIMAN ILAA YAUMID-DIYN. ALLAAHUMMAS-QINAAL-GHAYTHA WALAA TAJ-‘ALNAA MINAL-QAANITWIYN. ALLAAHUMMA INNA BIL’IBAADI WAL-BILAADI MINAL-JAHDI WAL-JU’UU WAD-DHWANKI, MAA LAA NASHKUU ILLA ILAYKA. ALLAAHUMMA ANBITI LANAAZ-ZAR’A WA ADIR LANAAD-DHWAR’A, WA ANZIL ‘ALAYNAA MIN BARAAKATIS-SAMAA, WA ANBITI LANAA MIN BARAKAATIL-ARDHWI. WAKSHIF ‘ANNAA MINAL BALAAI MAA LAA YAKSHIF-U GHAYRUKA, ALLAAHUMMA INNAA NASTAGHFIRUKA INNAKA KUNTA GHAFAARA, FA-ARSILIS-SAMAA ‘ALAYNAA MIDRAARA”.

MAANA:

“Ewe Mola wa haki wee! Ijaalie mvua hii kuwa ni mvua ya rehema na wala usiijalie kuwa ni mvua ya adhabu, wala ya hilaki, balaa, bomoa bomoa wala gharika. Ewe Mola wa haki wee! Tunakuomba inyeeshe vilimani na kwenye mafungu ya mchanga, maoteo ya miti na ndani ya mabonde. Ewe Mola wa haki wee! Tunakuomba inyeeshe pembezoni mwetu na wala isinyeeshe juu yetu. Ewe Mola wa haki wee! Tunakuomba utunywesheleze mvua yenye kuondosha dhiki, yenye neema, yenye kuotesha, yenye kuingia ndani ya ardhi, yenye kuenea kila mahala daima mpaka siku ya Kiyama. Ewe Mola wa haki wee! Tunakuomba utuletee mvua na wala usitujaalie kuwa miongoni mwa wenye kukata tamaa. Ewe Mola wa haki wee! Hakika waja (wako) na nchi ina mashaka, njaa na dhiki kuu ambayo hatuna wa kumshitakia ila wewe tu. Ewe Mola wa haki wee! Tunakuomba utuoteshee mimea na utububujishie maziwa, utushushie miongoni mwa baraka za mbinguni na utuoteshee miongoni mwa baraka za ardhi. Na utuondoshee balaa ambayo hakuna awezaye kutuondoshea ila wewe tu. Ewe Mola wa haki wee! Hakika sisi tunakuomba msamaha, bila shaka wewe ni Mwingi mno wa (kutoa) msamaha. Basi tunakuomba utuletee mawingu yanyeshayo mvua nyingi”. Bukhaariy (967), Muslim (897), Abuu Daawoud (1169), Shaafiy (AL-UMMU 1/222) & wengineo-Allah awarehemu.

@moodyhamza

Facebook Notice for EU! You need to login to view and post FB Comments!