Hali Ya Mzee Majuto Tete

 


MWEZI Mei, mwaka huu, gazeti ndugu la hili, Ijumaa Wikienda liliripoti habari mbaya juu ya lejendari wa vichekesho Bongo, Amri Athman ‘Mzee Majuto’ kuwa katika hali mbaya kiafya, lakini kwa hali yake ilivyo kwa sasa anahitaji dua za Watanzania.

AFANYIWA UPASUAJI
Habari mbaya zilizolifikia Amani, mapema wiki hii zilieleza kuwa, Mzee Majuto yu kitandani kwa mara nyingine kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa uliosababisha afanyiwe upasuaji.
Chanzo makini kililieleza Amani kuwa, Mzee Majuto ambaye amezaliwa mwaka 1948, alilazwa kwa siku tano hospitalini huko mkoani Tanga akisumbuliwa na ugonjwa wa hernia (ngiri) ambapo ililazimu afanyiwe upasuaji ili kumsaidia kwenye tatizo lake hilo la muda mrefu.

Chanzo hicho kilieleza kuwa, kufuatia tatizo hilo, Mzee Majuto amekuwa akitumia dawa za hospitalini na zile za kienyeji, lakini hakuna unafuu wowote anaoupata.
“Kuna kipindi alilazwa hapo katikati, alipopata nafuu aliruhusiwa lakini wiki iliyopita alibanwa sana na unajua yule mzee alikuwa anaogopa kufanyiwa operesheni ila kutokana na afya yake imebidi akubali tu,” kilisema chanzo chetu hicho na kuongeza:
“Kimsingi Mzee Majuto anahitaji dua za mashabiki wake na Watanzania kwa jumla.”

 

MKE WA MZEE MAJUTO AFUNGUKA
Baada ya kupata habari hizo, Amani lilimtafuta msanii huyo kwa njia ya simu yake ya kiganjani ambapo ilipokelewa na mkewe, Aisha Yusuf ambaye alithibitisha mumewe kuumwa.

Mama Majuto alisema kuwa, hadi wakati anazungumza na gazeti hili alikuwa yupo na mumewe katika Hospitali ya Tanga Central Health Centre (TCHC) ambako alilazwa kwa siku tano na kufanyiwa upasuaji.

“Ni kweli Mzee Majuto anaumwa ndiyo maana nimepokea simu yake, nipo naye hapa hospitalini, anasumbuliwa na ugonjwa wa hernia ambao umeibuka na kumuanza tena.
“Tunamshukuru Mungu kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji hivyo Watanzania na mashabiki wake waendelee kumuombea na Mungu akipenda hivi karibuni tu atarudi mzigoni, watarajie mambo mazuri kutoka kwake,” alisema mama Majuto.

Amani lilipoomba kuzungumza na Mzee Majuto mwenyewe, mkewe alisema alikuwa usingizini kwani alitakiwa apumzike baada ya upasuaji.
“Nitamfikishia pole lakini haruhusiwi kuzungumza, anatakiwa kupumzika,” alisema mama huyo na kuongeza:
“Hata hivyo, tumeambiwa tutaruhusiwa kutoka hapa hospitalini muda wowote.”

MASHABIKI WAMMISS
Wakiongea na gazeti hili, baadhi ya mashabiki wa staa huyo walisema kuwa, wamemmiss sana kwenye fani yake ya uigizaji na kumuomba Mungu afanye miujiza na amrejeshee afya yake.
“Kwa kweli tumemmiss sana, tunaamini atapona na kurejea kwenye hali yake ya kawaida,” alisema mmoja wa mashabiki aliyejitambulisha kwa jina la Said Juma.

UGONJWA WA HERNIA
Hernia au ngiri ni aina ya ugonjwa ambao humpata mtu baada ya misuli au kuta za tishu mwilini zinazoshikilia au kubeba viungo (organs) fulani kupoteza uimara au kuwa na uwazi (opening) hivyo kusababisha viungo hivyo kutoshikiliwa ipasavyo.

Miongoni mwa vitu vinavyoweza kumsababisha mtu kupata hernia ni pamoja na kuwa na uzito mkubwa au kuongezeka uzito kwa ghafla, kazi ya kubeba au kunyanyua vitu vizito, tatizo la kukohoa au kupiga chafya kwa muda mrefu, ujauzito au matatizo yanayojitokeza kwa mwanamke wakati wa kujifungua.
Pia kuharisha au kuvimbiwa (constipation). Vitu hivyo humfanya mtu apate hernia ambayo husababisha afanyiwe upasuaji ili kumaliza tatizo hilo.

Source: Udaku