Msanii Stamina Anahitaji Tuzo.

Mwaka 1833 alizaliwa Alfred Nobel ambaye ni mwanzilishi wa tuzo zenye heshima kubwa duniani, tuzo za Nobel.

Tangu ilipoanzishwa tuzo ya Nobel watu mbalimbali wametunukiwa tuzo hiyo kama vile Albert Einstein, Niels Bohr, Max Planck, Mama Teresa, Nelson Mandela na wengineo. Tuzo ya Nobel ni tuzo ya fedha kwa ajili ya mafanikio ya pekee katika fani mbalimbali.

Tangu mwaka wa 1901 imetolewa kwa watu waliofaulu katika fani za fizikia, kemia, tiba fasihi na amani. Inaharifiwa kuwa tuzo hii ni ya kimataifa na mashuhuri kabisa duniani.

Mtu wa kwanza kushinda tuzo hii katika upande wa fasihi ni Theodor Mommsen ambaye alikuwa mwanahistoria na mwandishi kutoka nchini Ujerumani. Mwafrika wa mwisho kushinda Tuzo ya Nobel ya fasihi alikuwa raia wa Afrika Kusini J.M. Coetzee mwaka 2003, aliyebadili uraia kuwa Muaustralia.

Karibu Stamina

Licha ya makala haya kuzungumzia muziki wa rapper Stamina, nimeamua kuanza kwa historia fupi ya tuzo za Nobel kutokana na ukubwa wake, ukongwe, heshima na namna zilivyojitanua kwa vitu vingi hadi fasihi.

Stamina ni sehemu ya fasihi pia kwa namna anavyowasilisha muziki wake katika Bongo Flava, ana heshima yake aliyojitengeneza kwa kipindi ambacho amesikika. Naitazama kazi yake aliyoifanya kwa jicho la tatu, ameweza kuwa bora zaidi katika ngoma za majibizano katika muziki wa hip hop Bongo.

Kwa kipindi cha miaka minne ameweza kufanya ngoma za aina hiyo zaidi ya tano, uzuri ni kwamba asilimia kubwa ameshirikishwa, maana yake ni kwamba kwa sasa msanii wa hip hop anayetaka kufanya battle song lazima jina Stamina ligonge kichwani mwake, tutazame hizi kazi kwanza.

Stamina Vs Nay wa Mitego

Baada ya Nay Mitego kufanya vizuri na kolabo zake mbili na Diamond ‘Muziki Gani, Mapenzi Pesa’ ambazo pia zilikuwa katika mfumo wa battle aliamua kubadili upepo kwa kufanya kolabo na msanii wa hip hop.

Utakumbuka katika ngoma ya muziki gani katika majibizano na Diamond, Nay alisimama kama msanii anayewakilisha kundi la muziki wa hip hop wakati Diamond akiwakilisha Bongo Flava.

Hata hivyo katika Huko Kwenu vipi Nay amewakilisha wasanii waliokimbia hip hop kwa madai hailipi na kuamua kuimba kama suluhisho la kufanya muziki wao kuwa biashara, huku Stamina akiwakilisha kundi la wale wanaoamini katika misingi ya hip hop na kuamini muziki wowote unaweza kuwa biashara.

Nay: Mnajifanya mnafanya ngumu wakati hamna majukumu, wengi wenu wala ndumu na bado mnaishi kwenu/

Usibishane na mimi wewe bado unasoma, show zenu bei rahisi hata kwa bia mnafanya/

Stamina: Hip hop inahitaji vichwa siyo kunywa mchuzi pweza, brother huku kwetu ulifichwa umesepa sababu ya kumezwa/

Ama kweli nimeamini wanawake mkiwezeshwa mnaweza/

Kama umenishindwa mimi je Fiq Q utamuweza?

Ngoma hii iliyotoka July 2014 producer aliyehuska katika mdondo ni Mr. T Touch ambaye hapo awali alikuwa akifanya ngoma za Nay wa Mitego katika studio ya msanii huyo

Stamina Vs Young Killer

Kama kumbukumbu zangu zipo sawa bila shaka hii ndio ngoma ya kwanza kwa Stamina kufanya battle ambayo wengi waliielewa zaidi, baada ya hapo kilichofuata ni mfululizo wa ngoma za aina hiyo.

Young K: Ukiniacha tunda mnafiki utakula maganda, hata ukifa umelala hawezi ukazikwa juu ya kitanda/

Stamina: Sijilindi na ustaa najikinga na ukimwi, naogopeka kila mtaa kama nilizini na zimu/

Ngoma hii ilitoka August 2013 ilisumbua vilivyo na kwa upande wa pili ilizidi kumtangaza Young Killer ambaye ilikuwa ni ngoma yake ya pili kutoa official baada ya Dear Gambe, pia wasanii hawa wamekutana katika ngoma kundi la Mtu Chee ‘Mtu Tatu’ Young Killer akiwa ameshirkishwa.

Stamina Vs Roma

Baada ya kufanya baadhi ya ngoma pamoja wakaamua kupiga hatua moja mbele zaidi kwa kuanzisha umoja wao waliopa jina la Rostam.

Kuzaliwa kwa Rostam kukaleta baraka ya ngoma Hivi Ama Vile ambayo kwa sasa ni miongoni mwa ngoma chache za Bongo Flava zinazokimbiza mtaani.

Eti muziki una team haya tema Kiba mpo wapi, team hazijengi hata Wasafi wakijenga masaki/

Mimi Wema wewe boya unalipi la kusema, mimi Zari nipo zangu Madala na ninaishi vema/

Ngoma hii ambayo ilitoka Augost mwaka huu chini ya producer Mr. T Touch ni ya tatu kwa wasanii hawa kufanya pamoja baada ya Mwanakondoo ya Roma na Mmeniroga Remix ya Stamina

Stamina Vs Joh Maker

Hapa vinakutana vichwa viwili kutoka Morogoro, ni baada ya Joh Makeer kushinda katika mashindano ya Super Nyota.

Katika ngoma hii ni watu wanaopeana taarifa za sehemu mbili tofauti lakini sehemu hizo ni katika muziki na kuonyeshana uwezo wa kupanga punch line na kutirika nazo.

Stamina: Nakula unga ila sembe South sipigi mbizi, mimi ndio genius wa mirembe niliyefeli ule mtihihadi wa uchizi/

Mjeshi nisiye na gwanda kuruta uteleza kipa, wanauliza mimi jogoo la shamba huku mjini nawiki vipi/

Yanukuu mema ila nina mengi ya kusema, mpo wengi ila Joh Maker nina tenzi za kuchana/

Nina ujenzi wa kunena, pata mwenye mema, na kama ukitaka elimu mimi ndio shule ya kusoma/

Stamina Vs Nacha

Nacha ni msanii wa hip hop ambaaye kwa sasa anakuja vizuri na kazi ambazo anazitoa zinaonyesha kuwa atafika mbali, ukiachilia mbali ngoma hii aliyofanya na Stamina kama umebahatika kusikia kazi yake aliyotoa na G Nako ‘Boss Mpya’ utakubaliana na hilo.

Katika ngoma ‘Subiri Kwanza’ aliyomshirikisha Stamina amekuwa wakibattle katika mada ambayo ni msanii underground ambaye anataka kutoka ila anahitaji kujua baadhi ya mambo ambayo yanaendelea katika game.

Wakati wa kuuliza na kujibiwa katika mtindo wa punch line wanajikuta wakizungumza na mambo mengine ila ndani ya muziki.

Nacha: Nimekumbuka kuna stori za unafiki, zinavuma eti Joh Makini anaandikiwa na Nikki/

Mimi siafiki Kiba kujiita king, wakati king ninayemjua mimi ni King Kiki/

Stamina: Wanaosema hip hop hailipi hizo stori za uogo, kuna marapa hawalipi so dogo fungua ubongo/

Acha masihara usikae ukisubiri kiki, hakuna muziki wa biashara fanya biashara ya muziki/

Best Rapper Battle

Baada ya kuainisha kazi hizo kadhaa bila shaka msanii wa aina hii kuna kitu cha pekee yake au heshina anastahili kutokana na kazi zake.

Ubaya ni kwamba muziki wetu kwa sasa hauna tuzo na hata zikiwepo huwa haziangalii mambo ya ndani zaidi kama haya zaidi ya kufuata trending ya kipindi husika. Hivyo basi, nitamatishe kwa kuieleza tasnia ya muziki bongo Stamina na wasanii wa aina yake kuna kitu cha zaidi wanastahili ila kuondoa ule usemi ‘Muziki Tunaudai’.Nawasilisha.

Source: Bongo 5.com