Mambo muhimu ya kuzingatia ili kuwa na afya bora

Ni wakati wa matazimio mapya. Miongoni mwa maazimio(resolutions) zinazoongoza ni pamoja na ile ya kuishi maisha yaliyo na afya bora zaidi na
furaha. Afya na furaha ni mambo mawili makubwa sana katika maisha yetu.Ukichunguza sana takribani kila kitu tunachokifanya ni katika mpambano wa kimaisha wa kuwa na afya bora zaidi na kuwa na furaha.
 Sote tunakubaliana kwamba afya bora ndio kila kitu.Ukiwa tajiri kupindukia halafu ukawa na afya mgogoro,ni wazi kwamba huwezi kuzifurahia hizo hela zako.
Yafuatayo ni baadhi ya mambo unayoweza kuyafanya ili kuwa na afya bora katika maisha,
.Lakini kabla sijaendelea mbele sana,naomba niweke wazi kwamba afya bora haihusu kula vizuri na mazoezi peke yake bali pia fikra chanya(positive
attitude). Kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba siku zote unakuwa na mawazo chanya na pia kuwa karibu zaidi na watu wenye mawazo chanya.
1.Kunywa Maji kwa wingi-
Bila shaka unakumbuka msemo “Maji ni Uhai”.Hiyo ni kweli kabisa.Maji ni uhai sio tu kwa mazingira yetu na dunia kwa ujumla bali pia kwa afya au
miili yetu.Maji ni kitu muhimu sana kwa afya zetu.Asilimia 60% ya miili yetu imetengenezwa au imesheheni maji. Maji yanahitajika kwa ajili ya kuondoa takataka au vitu visivyofaa kutoka mwilini.Maji ndio hubeba virutubisho na oxygen.
     Kiasi cha maji anachohitaji mtu kinategemea na mambo kadhaa kama vile unyevu(humidity) wa mahali ulipo,shughuli zinazohusisha mwili anazozifanya mtu na
pia uzito wa mwili.Pamoja na hayo,kwa wastani miili yetu inahitaji lita 2 na nusu mpaka 3 za maji.Vyakula tunavyokula
huchangia kama asimilia 20% za maji katika miili yetu.Kwa hiyo tunahitaji kunywa maji kiasi cha lita 2 mpaka lita 2.4 au glasi 8-9 za maji kwa siku.
    Njia rahisi ya kujua kama mwili wako una maji ya kutosha ni katika kuangalia mkojo. Mkojo wako unatakiwa kutokuwa na rangi(colorless) au
kuwa wa njano kidogo.Kinyume cha hapo ni ishara kwamba hauna maji ya kutosha mwilini.Njia nyingine kutambua ni pamoja na kukaukwa na midomo(lips) na hata ulimi na pia kupata kiasi kiduchu cha mkojo.
2.Pata Usingizi wa Kutosha:
Unakumbuka tulipokuwa wadogo wazazi wetu walisisitiza sana kwamba twende tukalale mapema ili tukue? Bila shaka walikuwa wanajua kwamba usingizi ni sehemu muhimu sana katika afya.
Ukiachilia mbali faida za usingizi kwa ajili ya afya za akili/ubongo wetu,usingizi au mapumziko ya kutosha ni muhimu kwa miili.Afya njema huenda sambamba na mapumziko.Ni wakati wa kuupa mwili nafasi ya kujijenga,kujiongezea nguvu na muhimu zaidi kuhakikisha kwamba tunakuwa na akili timamu. Pia ukosefu wa usingizi ni chanzo cha kuzeeka mapema.
3.Fanya Mazoezi-
Hili linaweza kupita bila maelezo ya ziada.Mazoezi ni muhimu sana kwa afya bora. Fanya mazoezi angalau mara tatu katika wiki.Jipatie muda wa kutembea japo kwa dakika 30. Kama inawezekana nenda Gym.Badala ya kupanda lifti pale kazini kwako au mitaani,tumia ngazi za kawaida.Egesha gari lako mbali kidogo na unapokwenda ili upate nafasi ya kutembea nk. Muhimu zaidi ni kuchagua aina ya mazoezi unayoipendelea. Mazoezi hayatakiwi kuwa adhabu.
    Faida za mazoezi ni pamoja na kujiepusha na magonjwa mbalimbali,kupunguza unene(bila shaka unajua kwamba unene kupindukia sio afya bali ni ugonjwa na sababu kubwa ya maradhi mengine)
4.Kula Matunda Kwa Wingi
-Matunda ni chanzo kizuri sana cha madini na vitamins ambazo miili yetu inahitaji sana kwa ajili ya afya bora. Unajua kwamba machungwa,kwa mfano, yana faida kubwa zaidi kiafya kuliko vidonge vya Vitamin C unavyobugia kila leo? Aina mbalimbali za matunda ambayo yana virutubishi vingi zaidi kiafya ni Parachichi(Avocado),apple,matikitimaji(cantaloupe),Zabibu(Grapefruit),Kiwi,Guava,mapapai,machungwa, strawberries nk.
5.Kula mboga za majani
 Kama ilivyo kwa matunda,mboga za majani(vegetables) ni muhimu sana kwa afya zetu. Wataalamu wa afya wanashauri kwamba tule aina 5 mpaka 9 za mboga za majani na matunda.Jitahidi kupata angalau zaidi ya aina 5 za mboga za majani na matunda.
6.Punguza Kula Vyakula vya Makopo
 Kutokana na jinsi dunia inavyozidi kwenda mbio,watu wengi huwa tunakosa muda wa kupika.Matokeo yake tunakimbilia kwenye vyakula vya kwenye makopo ambavyo ndivyo vimejaa katika maduka na ma-supermarket. Jitahidi kuviepuka vyakula hivyo kwa kadri unavyoweza.Mara nyingi vyakula vya
makopo huwa na ingredients ambazo hazifai kwa afya zetu.Kwa mfano,vingi miongoni mwa vyakula hivyo huwa na chumvi nyingi kitu ambacho ni chanzo
cha High Blood Pressure na maradhi ya moyo. Unaposhindwa kabisa kujizuia kununua vyakula hivyo vya makopo jaribu kuangalia ambavyo havina sukari au chumvi.
7.Jipende
 Kama nilivyodokeza hapo mwanzo,afya bora huenda sambamba na afya ya akili/ubongo.Njia mojawapo ya kupata afya hiyo ni pamoja na
kujipenda.Pengine unajiuliza,kuna mtu ambaye hajipendi? Ukweli ni kwamba pengine ni kweli kwamba hakuna mtu ambaye hajipendi.Tofauti inakuja pale mtu anapofanya vitu ambavyo ni kinyume kabisa na mapenzi ya mwili.
Mfano,uvutaji sigara,unywaji pombe kupindukia,kutojisafisha mwili wako kwa mfano kuoga,kupiga mswaki na pia kupumzika nk.Hizo zote ni tabia
ambazo zinaweza kuonyesha jinsi ambavyo hujipendi au huupendi mwili wako.Kama unaupenda utautumia vibaya au kuuharibu?