Lulu Asema Kanumba Alinikimbiza na Panga.

MSANII wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu ameanza kujitetea katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akieleza alichokuwa akifanyiwa na marehemu Steven Kanumba.Akitoa utetezi wake katika kesi hiyo ya kuua bila kukusudia, Lulu amesema Kanumba alikuwa akilewa na kumpiga na kwamba Kanumba aliwahi alimpiga kwa panga mapajani na akapelekwa Hospitali ya Mwananyamala.“Nilipofika kwa marehemu ‘Kanumba’ nilimkuta yupo kwenye dressing table, nilikaa kitandani kwa kuwa hapa kuwa na sehemu ya kukaa.“Sijasababisha kifo cha Kanumba kwa namna yoyote ile. Umbo langu lilikuwa dogo hivyo mimi ndiyo nilikuwa nashambuliwa. Kama marehemu asingeanguka labda angenidhuru. Kanumba alikuwa kama mlezi wangu, tulianza mahusiano miezi minne kabla ya kifo chake,” amesema Lulu.

“Nilikuwa nataka kutoka ila marehemu (Kanumba) alinikataza, alikuwa hataki nitoke, nilipomwambia natoka na marafiki zangu alinikimbiza na taulo na mimi nilikuwa naogopa kupigwa, mara nyingi alikuwa ananipiga kila akilewa na sio kwa akili zake. Alipoona simu yangu inaita akahisi ni simu ya mwanaume akasema kwa nini naongea na simu ya mwanaume mbele yake? Marehemu akaingia uvunguni akatoa panga akasema leo nakuua huku akinipiga na panga kwenye mapaja”, ameelezea Lulu. Lulu ameendelea kusimulia…. “Marehemu alianguka mwenyewe na kujigonga kwa nguvu na kuinuka akitapatapa, nilimwambia Seth kuwa Kanumba amedondoka na akajaribu kumuamsha hakuamka, akasema anaenda kumuita daktari, alivyosema anaenda kumuita daktari na mimi nikaondoka nikiogopa anaweza akaamka akaanza kunipiga. Niliondoka nikawasha gari kuelekea Coco Beach kutuliza akili”.

Muigizaji huyo ameendelea kusimulia kwamba … “Nilivyofika Coco Beach meseji zilianza kusambaa kuniuliza kuwa nasikia Kanumba amefariki, nikampigia Kidume ambaye ni rafiki yake Kanumba kumuuliza Kanumba yupo hospitali gani niende kumuona, akaniambia wewe usije hospitali, niambie uko wapi, tukakubaliana tuonane Bamaga. Tulivyokutana Bamaga alikuwa kama anataka kuongea na mimi ghafla wakaja askari kunikamata.“Na kunipeleka Oysterbay polisi, nilipofika Oysterbay nilikuta watu wengi sana niliyemtambua ni Ray. Nilijua Kanumba amefariki nikiwa polisi. Nilipomkuta Ray Oysterbay polisi nikajua Kanumba amekamatwa kwa sababu ya makelele niliyokuwa nayapiga kule nikajua watu walisikia.“Kwa namna yoyote ile mimi sijasababisha kifo cha Kanumba, na mimi ndiye nilieshambuliwa na marehemu,” ameeleza Lulu.

Maswali kutoka kwa wakili wa serikali

Wakili wa Serikali: Wewe na Kanumba mlianza mahusiano kwa muda gani?

Lulu: Miezi minne kabla ya kifo chake.

Wakili wa Serikali: Inamaana Kanumba alikukimbiza na taulo mpk nje halikuanguka?

Lulu: Ndiyo, alinikimbiza akiwa peku na taulo.

Source: Global Publishers.