Kuhusu Watanzania 11 waliokamatwa Johannesburg South Africa

Ni taarifa kutoka Johannesburg South Africa ambako Wanaume 11 ambao ni raia wa Tanzania wamekamatwa na Polisi na kufikishwa Mahakamani wiki hii. (hiyo picha hapo juu ni Askari wa South Africa wakiwa kazini na haihusiani na tukio la leo)

Radio na Mtandaoni Johannesburg wiki hii kumeripotiwa kuwa kosa lililofanya Wanaume hao 11 kukamatwa na Polisi ni kumbaka Mwanamke mjamzito mwenye umri wa miaka 22 aliyekua akitoka kazini saa kumi na moja alfajiri.

Mwanamke huyo alikua akitoka kazini na Mfanyakazi mwenzake ambaye ni Mwanaume ambapo ghafla walivamiwa na kundi la Wanaume wenye silaha za moto na wakamvuta Mwanamke huyo kabla ya kumpiga Mfanyakazi mwenzake ambae baadae alifanikiwa kutoroka.

Baada ya Mfanyakazi huyo kutoroka aliwapigia simu Polisi na wakafanikiwa kuwahi eneo la tukio na kukuta Wanaume hao wakimbaka kwa zamu Mwanamke huyo mwenye ujauzito wa miezi mitatu.

Picha iliyotolewa na Polisi kuhusu vijana hao 11 baada ya kufikishwa kituo kikuu cha Johannesburg.

Polisi wapatao kumi waliingia kwenye jengo tukio lilikofanyika na kumuokoa Mwanamke huyo aliyekua kwenye hali mbaya ambapo walimpeka Hospitali huku Watuhumiwa wakichukuliwa na kupandishwa Mahakamani siku ya Jumatano.

Hii sio mara ya kwanza kwa Watanzania kuhusishwa na headlines mbaya kwenye jiji hilo la Johannesburg ambapo Polisi wa jiji hilo waliwahi kuiambia millardayo.com na AyoTV Watanzania hushikwa mara kwa mara lakini makosa yao huwa ni kuuza ama kukutwa na bangi.


Mmoja wa Polisi hao alitaja maneno ya kiswahili kama vile ‘Mjomba, bangi na mambo vipi‘ akisema alijifunza maneno hayo machache baada ya kuyasikia yakirudiwa kuzungumzwa mara kwa mara na Watanzania wanaoshikiliwa kituoni.

South Africa ni miongoni mwa nchi chache ambazo Watanzania huruhusiwa kuingia bila kibali cha kuingia, kuishi au kutembelea nchi husika (VISA) ambapo anachotakiwa kuwa nacho Mtanzania yeyote ili kuingia kwenye taifa hilo ni Passport peke yake.

Baadhi ya Raia wa South Africa kwenye mitandao ya kijamii waliandika maoni yao wengine wakisema ‘ndio maana sipendi wageni, wamesafiri koooote kutoka Tanzania kuja kubaka dada zetu?’

Source: Millard ayo