je ni kweli Kutokana na kazi zao, Malaika wengi tunaishi nao …

Malaika ni katika waja na viumbe wa Allah(SW) walioumbwa kutokana na nuru. Tunafahamishwa katika hadithi ifuatayo kuwa: Aysha (r.a.) amesimulia kuwa Mtume (s.a.w.) amesema: Malaika wameumbwa na nuru na majini wameumbwa kutokana na ndimi za moto na Adamu ameumbwa kwa udongo kama ilivyoelezwa kwenu (katika Qur’an). (Muslim) Na katika Qur’an tukufu, Allah(SW) anatubainishia kuwa, katika maumbile yao halisi, malaika ni viumbe wenye mbawa. “Sifa zote njema ni za Allah, Muumba wa mbingu na ardhi. Aliyewafanya malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbili-mbili, na tatu tatu, na nne nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo. Bila shaka ni mwenye uweza juu ya kila kitu”. (35:1)

Je malaika wanaishi wapi?

Katika Qur,an tunafahamishwa kuwa Malaika wanayo makazi maalumu lakini si hapa duniani. Allah(SW) anawanukuu malaika wakisema: Hakuna yoyote miongoni mwetu ila anapo mahali pake mahususi. Na kwa yakini katika sisi wapo wajipangao safu. Na wako katika sisi wamtukuzao(Mwenyezi Mungu) (37:164-166)

Kutokana na kazi zao, Malaika wengi tunaishi nao humu humu duniani na wako nasi muda wote.Kila mtu ana malaika wawili wenye kuandika amali zake. Hakika juu yenu kuna wenye kuwatunza, malaika watukufu wenye kuandika.Wanayajua yote mnayoyatenda(82:10-12) Aidha, tunafahamishwa katika Qur,an kuwa kila mmoja wetu ana kundi la malaika mbele na nyuma yake. Ana (kila mtu) kundi (la malaika) mbele yake na nyuma yake.Wanamlinda kwa amri ya Mwenyezi Mungu. (13:11)

Kwanini hatuwaoni Malaika?

Pengine mtu aweza akauliza kuwa kama tumezungukwa na malaika mbele na nyuma, kulia na kushoto, kwanini basi hatuwaoni? Jibu ni kwamba, mwanadamu yupo kwenye mtihani. Mtihani wenyewe ni kufanya mema kwa kutaraji malipo ya Allah(SW) na kuacha maovu kwa kuogopa adhabu zake. Ametukuka yule ambaye Mkononi mwake umo ufalme(wote); naye ni mwenye uweza juu ya kila kitu. Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni; ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Naye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha(67:1-2) Malaika ndio wasimamizi wa mtihani huu, na wamefanywa wasionekane machoni petu ili kila mtu atumie uhuru wake wa ama kumuogopa Allah(SW) kwa kutenda mema au kumkufuru Allah(SW) kwa kumuasi.

Lau malaika wangelionekana, watu wengi wangelitenda mema kinafiki(ria) badala ya kufanya kwa ikhilaswi. Mfano wake, ingekuwa kama vile watu wenye dhamira za kufanya uhalifu wanavyojidai watu wema pale wanapokuwepo askari waliovalia rasmi. Utendaji kazi wa malaika ni kama mashushushu au askari kanzu. Mtu muovu anapanga na kutenda maovu akidhani yupo peke yake, kumbe malaika wapo wanaandika. Na ndiyo maana muovu atakapoona kila jambo lake limerikodiwa, atashangaa siku ya kiama kuwa alijulikanaje? Na madaftari yatawekwa mbele yao.

Utawaona wabaya wanayaogopa kwasababu ya yale yaliyomo; na watasema: “Ole wetu! Namna gani madaftari haya! Haliachi dogo wala kubwa ila yamelidhibiti.Na watakuta yote yale waliyoyafanya yamehudhuria hapo; na Mola wako hamdhulumu yeyote(18:49) Siku mtu atakapowaona malaika Kuna siku na muda maalumu ambapo kila mtu binafsi ataanza kuwaona malaika katika umbile lao halisi.

(a) Siku ya kukata roho Hii ni siku na saa ambayo dakika chache baada ya hapo mtu hukata roho na kuiaga dunia. Kwa watu wema, watakuja malaika wa kuwaliwaza: ……Hao huwateremkia Malaika “msigope wala msihuzunike, na furahini kwa pepo mliyokuwa mkiahidiwa. Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na (huku) katika Akhera……”.(41:30-32) Watu wanaotenda maovu watapata mshituko mkubwa na kujawa na huzuni kubwa mno pale watakapowaona Malaika. Watasikitika sana kwa jinsi walivyokuwa wakijidanganya nafsi zao, wakatenda maovu kwa kudhania kuwa hakuna Malaika wanaorekodi matendo yao waliyokuwa wakiyafanya hadharani na mafichoni. Watafadhaika na kusema: ….Mola wangu! Nirudishe(duniani). Ili nifanye mema sasa badala ya yale niliyoyaacha. (Malaika watamwambia): “Hapana! Hakika hili ni neno tu analosema yeye(mtu muovu)….(23:99-100)

(b) Siku ya kiyama Kuanzia pale mtu anapowaona malaika hakutakuwa tena na kizuizi cha kutowaona kama ilivyokuwa hapa duniani. Kuonekana Malaika siku ya kiama itakuwa ni ishara mbaya kwa watu waovu kuwa umeshafika wakati wa wao kuhukumiwa na Allah(s.w) na kuanza kutumikia adhabu za kudumu katika Moto wa Jahannam. Qur’an inatufahamisha kuwa: Siku watakayowaona Malaika haitakuwa furaha siku hiyo kwa wenye makosa; na watasema:”(Mungu) atuepushie mbali adhabu hii iliyotukabili(lakini haitawafaa kitu dua hiyo)(25:22)

(c) Motoni na Peponi Malaika watahudhuria katika uwanja wa hukumu siku ya Kiyama. Kila mtu atawaona wamejipanga safu wakisubiri amri ya Mwenyezi Mungu. Siku ambayo zitasimama Roho na Malaika safu safu; hatasema siku hiyo ila yule ambaye(Allah) Mwingi wa rehema amempa idhini, na atasema yaliyo sawa(78:38) Wakipewa amri na Allah(s.w) malaika watawakamata waovu na kuwachungachunga kuelekea motoni kuadhibiwa. Na waliokufuru watapelekwa katika Jahannam makundi makundi mpaka watakapoifikia; itafunguliwa milango yake; walinzi wake(malaika) watawaambia: Je! hawakukujieni Mitume miongoni mwenu wakikusomeeni aya za Mola wenu na kukuonyeni juu ya makutano ya siku yenu hii(39: 71)

Watu wema watasindikizwa na malaika mpaka kwenye pepo tukufu, na malaika wa huko watawakaribisha. Na walinzi wake(malaika) watawaambia: Amani juu yenu, furahini, na ingieni humu mkae milele(39:73)

Sifa za malaika
Ni viumbe watiifu wasiomuasi Allah(SW)

Malaika ni viumbe watiifu kwa Allah(SW). Wakipewa amri ya kumuadhibu mtu muovu, hawagomi wala kumuonea huruma mtu huyo. Enyi mlioamini! Ziokoeni nafsi zenu na nafsi za watu wenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Juu yake kuna Malaika wakali wenye nguvu.Hawamuasi Allah(SW) katika yale anayowaamuru, na wanatekeleza vile walivyoamrishwa.(66:6) Wana elimu ya kutosha kutekeleza majukumu yao Malaika wana elimu inayowawezesha kutekeleza majukumu yao bila ya kubabaisha. Elimu waliyopewa malaika ni sehemu ndogo sana katika ujuzi wa Allah(SW). Na wenyewe walikiri mbele ya Allah(SW) Wakasema: Utukufu ni wako! Hatuna elimu ila ile uliyotufundisha, bila shaka wewe ndiye mjuzi na mwenye hekima(2:32)

Hawana jinsia

Malaika hawana jinsia ya kike wala ya kiume. Qur’an inawakosoa watu wanaodhani kuwa malaika ni wanawake. Inahoji: Na wamewafanya malaika ambao ni waja wa Mwingi wa Rehma kuwa ni wanawake. Je wameshuhudia kuumbwa kwao(43:19).

Ni viumbe wenye mbawa

“Sifa zote njema ni za Allah, Muumba wa mbingu na ardhi. Aliyewafanya malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbili-mbili, na tatu tatu, na nne nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo. Bila shaka Allah ni mwenye uweza juu ya kila kitu”. (35:1)

Huweza kujimithilisha umbile la mwanadamu Malaika huweza kujimithilisha kuwa kama wanadamu. Hufanya hivyo pale wanapotumwa na Allah(SW)kuleta ujumbe kwa watu maalumu. Kwa mfano, Bibi Maryam, mama yake nabii Isa(a.s), alijiwa na malaika katika umbo mithili ya mwanaume. Na mtaje katika kitabu, Maryam, alipojitenga na watu wake katika upande wa mashariki. Tukampelekea Muhuisha sharia Yetu(Jibril) akajimithilisha kwake kwa sura ya binaadamu aliye kamilifu. (19:16-17)

Lengo la kuumbwa malaika

Lengo la kuumbwa malaika ni kumtumikia Allah(SW). Katika kutekeleza lengo la kuumbwa kwao, malaika hawana hiyari katika kutekeleza amri za Allah(SW), hufanya mambo yote vile anavyotaka Allah(SW). ..Hawamuasi Allah(SW) katika yale anayowaamuru, na wanatekeleza vile walivyoamrishwa.(66:6)

story@moodyhamza