Serikali imewataka wananchi kuanzisha desturi ya kununua kazi za wasanii, kwakuwa ndiyo njia pekee inayoweza kuwanufaisha kwa kazi wanazozifanya.
Wito huo umetolewa wiki hii na Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Prof Elisante Ole Gabriel wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa tovuti a Afro Premiere, iliyoanzishwa kwa lengo la kuuza video za muziki za wasanii.
Alisema mpango huo unaweza kuwa ni moja ya mikakati muhimu ya kupambana na wezi wa kazi za wasanii, kwakuwa video za muziki zitakuwa zikipatikana kwenye mtandao huo peke yake kwa kipindi maalum na hivyo kuingiza pesa zinazoenda kwa msanii, serikali na watayarishaji moja kwa moja.
Pia alidai kuwa kwakuwa Afro Premiere itakuwa ikiweka nyimbo za Kiswahili zaidi, itasaidia kukikuza zaidi Kiswahili, ambacho ni cha 10 kati ya lugha elfu sita duniani na kuahidi kupitia wizara ya mambo ya nje, wizara yake itawaunganisha na Watanzania waliopo nje ya nchi.
Prof Ole Gabriel amewataka wasanii wao wenyewe kuunga mkono mpango huo sababu ndio njia pekee ya kuufanya ufanikiwe.
“Mpango huu utafanikiwa kama ninyi mkiwa sehemu ya mpango huu, kama ninyi wenyewe tena mkianza kuwa na kona kona na kuupiga vita, basi mpango huu utaonekana feki na utashindikana,” alisema.
Hadi sasa kuna video mbili mpya zilizowekwa kwenye Afro Premiere ambazo ni Go Low ya G-Nako na Jux pamoja na K wa Roma na Baghdad. Mashabiki wanaweza kununua nyimbo hizo kwa shilingi 300 tu kwa kutumia simu zao.
SOURCE: TEENTZ