Ni jambo zuri na la kheri kumkumbuka mtu unayemfahamu, unayemmiss na hata unayempenda, maana hilo ndilo Mwenyezi Mungu ametufundisha.
Katika barua yangu ya leo, nimemkumbuka mdogo wangu, dada yangu, ambaye amebahatika kujipatia jina mjini baada ya kuonekana kwenye video za wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya, wenyewe wanajiita mavideo queen, Gift Stanford maarufu kama Gigy Money.
Hii ni mara yangu ya kwanza kukuandikia barua, ingawa vioja vyako nimekuwa nikiviona sana kwenye vyombo mbalimbali vya habari, hasa mitandao ya kijamii na magazeti. Nikaanza kuwaza na kuwazua, inakuaje kwa mtindo wa picha za utupu ambazo umekuwa ukizipiga, hivi una wazazi kweli?
Una kaka, dada, shangazi, wajomba, baba wadogo na wakubwa kweli? Pamoja na kwamba huu ni ulimwengu wa digitali, sidhani kama huyu binti anastahili kufanya anavyofanya, maana ni kama vile kichwa chake hakijatulia vizuri. Na inanishangaza pia kama mdogo wangu huyu bosi wake ni mtu wa namna gani, maana hata kama haya ni maisha binafsi, baadhi ya mambo yanaharibu ‘image’ ya kampuni anayoifanyia kazi.
Pengine ni kama vile watu wa masoko wanavyosema, biashara matangazo. Huenda kuna biashara nisiyoijua anaitangaza, lakini naona kuna athari kubwa zaidi ya matangazo yake hayo kuliko faida anayoitaraji. Mimi kama kaka yako, naomba nikupe ushauri huenda ukakusaidia siku zijazo. Wewe mwenyewe unaweza kuona kuwa ni ujanja kupiga hizo picha na kuzitupia kwenye mitandao, kwa sababu hivi sasa wale wanaume wakware watakutafuta na kumalizana, hivi unajua kesho itakuwaje?
Sasa hivi unaweza usione tatizo, lakini amini ninachokuambia, kesho na keshokutwa huwezi kuolewa wewe. Nani atataka kuoa mwanamke wa aina yako, kama leo hii umeshafikisha zaidi ya umri wa miaka 18 unajitandaza mitandaoni, utashindwa kufanya hivyo ukiwa na umri wa kuolewa?
Na heshima ya mwanamke iko kwenye uhifadhi wa mwili wake, sasa kama wewe una heshima gani wakati kila mtu anaujua mwili wako ulivyo? Nahisi unasumbuliwa na ulimbukeni.
Hata hivyo, ulimbukeni siyo ugonjwa ni hali tu ya muda inayomtokea mtu yeyote, hasa anapokutana na vitu ambavyo hakuwahi kuwaza kama atakutana navyo. Pengine hakuwahi kuwaza kuwa siku moja watu watajua kuna Gigy, kama yeye alivyokuwa akiwasikia mastaa wakivuma wakati huo yeye akiwa hajulikani. Na kwa jina alilolipata, anadhani kwamba sasa yupo katika anga nyingine.
Hapana mdogo wangu, wewe bado mchanga sana katika anga za masupastaa, bado unahitaji make-ups za kutosha ili ukae meza kuu. Punguza ulimbukeni, kidogokidogo utakuja kukaa sawa. Jaribu kutafuta, hivi ni staa gani alifanikiwa katika maisha yake kwa sababu ya kupiga picha za utupu hapa Bongo?
Na niwakanye wadogo zangu wengine ambao mna mawazo ya kuja kuwa kama Gigy, heshima kubwa ya mwanamke iko ndani ya mwili wake, kadiri anavyouhifadhi ndivyo thamani yake inavyopanda.
Na kama wewe ni mzuri, utabakia kuwa hivyo hata kama utashinda ndani ya vazi la hijabu. Hata hao wanaume wenye tamaa za mwili hivi sasa, wanakudharau na kukuona kama chombo cha starehe kinachosubiri muda kuekspaya.
Na kwa akili hizi za kujiachia utupu namna hiyo, siamini kama unajua hata kuwekeza ili kufidia maisha ya muda mchache ujao utakapokuwa umekwisha habari yako.
                                              Source: Udaku