Njia Sita za Kumnasa Demu Mkali.

KUNA watu wamezaliwa wakiwa na hofu kubwa ya kuwaogopa mademu wazuri. Kuna mwingine akimuona demu mzuri mtaani, anajisemea kabisa kwamba; yule si taipu yangu, eti kisa kapendeza, msafi na anaonekana matawi fulani ya juu.

Mwanaume anatakiwa kujiamini, hakuna mwanamke duniani ambaye si saizi yako, kila demu unayemuona mtaani basi jua kwamba huyo ni saizi yako ndiyo maana Mungu kamuweka katika dunia hii na wewe kufanikiwa kumuona.

Leo nataka nikufundishe namna ya kumpata demu mkali, hata kama wewe ni muoga, unahisi kwamba mademu wa aina hiyo si taipu yako lakini naamini njia hizi zitakufanya kumpata kiurahisi kabisa na kufanya mambo yako, kama ni kupanga naye maisha au la.

TAFUTA JINA LAKE KWANZA

Unapomtaka demu mkali mtaani kwako, kitu cha kwanza tafuta jina lake. Hii itakusaidia kumshangaza. Wanawake wapo hivi, huwa hawapendi sana kujulikana, inapotokea msichana huyo ukaonana naye na kumuita jina lake, kwanza atasimama, atakuuliza umenijuaje? Nani kakwambia jina langu? Usiogope, kwanza tabasamu, hilo litamfanya kuona kwamba wewe ni mtu mzuri, jibu utakalompa, hakikisha linakuwa lile la kukutafuta baadaye.

Kwa mfano unaweza kumwambia: “Mbona nakufahamu! Wewe ni staa sana hapa mtaani, kila mtu anakujua!” ukimwambia hivyo, atataka kujua zaidi na zaidi, ni akina nani wanaomjua halafu mbona yeye siyo staa! Unachotakiwa kufanya ni kujiweka bize, mwambie ‘nitakwambia nimekujuaje ila kwa sasa kuna sehemu nawahi.’

Ukifanya hivyo itamfanya yeye kuwa na hamu ya kukutafuta. Hata ukimwambia akutafute baadaye, atakutafuta kwa lengo la kutaka kujua imekuwaje. Ukiona ameelekea kidogo, mwambie niachie namba yako, nitakwambia, si hilo tu, kuna mengi kuhusu wewe.

Nakwambia hivi, kwa hatua hiyo, hakuna msichana ambaye atakukazia namba yake, lazima atakupa.

USIMLETEE SANA SHOBO

Akikupa namba, usijifanye kuwa na haraka ya kumtafuta. Unachotakiwa kufanya ni kucheza na akili yake kwanza. Najua atakuwa na hamu ya kupata simu yako, kwa siku hiyo mkaushie mpaka kesho yake ndipo umtafute. Kuwa makini, usimpigie, wewe mtumie meseji, mwambie “Upo poa staa wangu wa ukweli?” atakachokifanya ni kuuliza wewe nani! Inawezekana akawa anajua, ila kwa mapozi ya kike ni lazima ajidai kuuliza. Mwambie ni yule mshikaji wa jana! Ongezea kwa kumwambia kwamba utamtafuta ukirudi kutoka kazini, hata kama huna kazi, jiongeze kidogo.

MPIGIE SASA, ANZA KUMSIFIA

Wanawake wanapenda sifa, wanapenda kusifiwa. Kitu cha kwanza mwambie kwamba kuna siku uliwasikia washikaji wakimzungumzia, kwamba demu fulani mkali, anajua kuvaa, ananukia vizuri, ukataka kumjua ndipo wakasema kwamba ni yeye. Hilo litamfanya kujiona anakubalika sana, kumbe watu wanamsifia mtaani, kumbe wewe unamuweka kwenye saiti yako.

Ukiwa unazungumza naye, jifanye mcheshi sana, mchekeshe, mwambie na wewe ulivyokuwa na hamu ya kumjua msichana huyo msafi na mrembo ndiyo maana ukaamua kumtafuta. Mpaka kufika hatua hiyo, ataanza kukukubali, kwa ucheshi utakaomuonyesha atakuona wewe mtu mzuri na mtakuwa mnaanza kuchati. Usimtongoze lakini muonyeshee dalili za kumtaka. Chati naye hata kwa wiki moja halafu fanya njia ifuatayo;

MUOMBE MTOKO WA KIZUSHI

Hapa simaanishi mtoko wa kwenda klabu au ule mtoko siriazi sana, kwanza mwambie wewe siyo mtu wa klabu ila unataka kumpeleka sehemu fulani hivi kwenda kunywa kahawa au juisi. Kwenye kumuomba mwambie utajisikia furaha ukiwa unatembea na demu mkali kama yeye, mwambie kila mwanaume anajisikia fahari akitembea na msichana anayependeza na kunukia vizuri kama yeye. Kwa sifa hizo za mara kwa mara, atakwambia anayo nafasi hivyo atakukubalia.

KUWA MAKINI KWENYE MTOKO WAKO

Demu yeyote anapenda mwanaume mchangamfu, jinsi utakavyomuonyeshea uchangamfu kwenye simu iwe hivyohivyo hata ukionana naye na kutembea naye. Usimuonyeshee akahisi yule wa kwenye simu ni tofauti na huyu.

NENDENI MNAPOKWENDA

Usitake kutumia sana pesa, usitake kuingia gharama kubwa kwani mademu wana kawaida ya kumsoma mwanaume siku ya kwanza tu. Kama vipi mwambie wakati wa kurudi mtembee kwa miguu, hii itakupa nafasi ya kuzoeana sana, hata kama akitaka mpande usafiri, mwambie mtachukua mbele, kwanza omba kutembea naye hata nusu kilometa. Katika maongezi yote usijisifie ila mfanye ajue unajua mambo mengi sana.

Jaribu kumwambia mambo ambayo unaamini hata yeye hayajui na angefurahi kuyajua. Mwambie kuhusu hadithi ya Romeo And Juliet, mwambie kuhusu Malkia Cleopatra alivyotetemesha kwa uzuri wake, mwambie mambo mengi ambayo utaamini kwamba hayafahamu ila angependa ayafahamu.

MALIZIA KWA KUMWAMBIA HIVI…

Mkiachana na kurudi nyumbani, mpigie simu, mwambie unamisi uwepo wake, ungetamani uwe naye tena, unaimisi harufu yake, mwambie ulikuwa karibu na ua kwa hivyo ile harufu yake imekupata hata wewe. Mchekeshe kidogo, mwambie unamisi tabasamu lake, mwendo wake wa twiga, mwambie unamisi uzuri wake, yaani huo ndiyo muda wa kumsifia mpaka ajione duniani hakuna mwanamke kama yeye. Ukifanya hayo, jua kwamba huyo mwanamke lazima akukubali kwani atahisi yupo na mtu sahihi. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine bomba zaidi.

Source: Udaku