NAY wa Mitego Apewa Onyo na Ustawi wa Jamii


DAR ES SALAAM: Kutokana na wanawake kadhaa kuwahi kujitokeza na kudai kwamba wamezaa na staa wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ lakini amewatelekeza, Idara ya Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam, imemuonya jamaa huyo na kumtaka kuwa makini katika hilo.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa maafisa wa ustawi wa jamii, Magomeni, Dar aliyejitambulisha kwa jina moja la Vaileth ambaye hakutaka kuanikwa cheo chake kwa kuwa siyo msemaji wa idara hiyo, alifunguka kuwa, suala la Nay kutelekeza watoto linaweza kumletea matatizo kama vile kifungo jela au kulazimishwa kumlea mtoto husika hadi akue na kuweza kujitegemea.

“Anachokifanya Nay siyo kitu kizuri kabisa kwani kwanza anawadhalilisha wanawake kwa kuzaa nao, halafu hawahudumii.

“Suala la kutelekeza watoto linaweza kumsababishia kifungo au kutoa matumizi kwa lazima kama wahusika, yaani wanawake waliozaa naye watachukua hatua za kisheria hivyo anatakiwa abadilike sana,” alisema afisa huyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, kulikuwa na kumbukumbu ya kuzaliwa ‘bethidei’ ya mtoto wa Nay aliyezaa na mwigizaji wa sinema za Kibongo, Skyner Ally ‘Skaina’ ambapo mwanamuziki huyo alimtakia heri katika kukua kwake huku akiweka picha na maneno kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Hali ilichafuka baada ya Skaina kuandika waraka mrefu kwenye ukurasa wake wa Instagram akiambatanisha na picha akiwa na mwanaye na kumtaka Nay kuacha kumshobokea mwanaye kwani ni miaka mitano sasa hajui anavaa nini, anakula nini wala anaishi vipi yeye amekalia kuposti picha za mtoto huyo tu wakati ni baba kwa jina tu.

“Baba jina anakufanyia promosheni kudanganya Watanzania kama ohoo my twin, sijui nanunua pisto, hata nguo ya ndani unayovaa hajui thamani yake, nimevumilia sana miaka mitano sasa nimejisikia kutapika na Mungu nakuomba unijalie maisha marefu, uwezo, nizidishie riziki, uzima na afya nikulee mwanangu aje akuone baadaye umekuwa waziri halafu alete pua yake sijui itakuwaje.

“Mungu akuweke uje uone mafanikio ya mwanangu, endelea na drama zako ila tafadhali shobo na mwanangu sitaki, unaposti picha za mtoto wangu za nini, sitaki shobo na mwanangu, je, wababa wanaojisifu kama wanawapenda watoto wao halafu hata hawajui mtoto anakula nini, anasoma wapi, anavaa nini, wapooo….

“Nilikuwa na dukuduku moyoni ndani ya miaka mitano nimeongea na limetoka ukweli, unamuweka mtu huru, kutwa kucha kuwadhalilisha wenzio ya kwako yanakushinda, usiwafunze wenzio, jifunze kwanza kwako,” aliandika Skaina.

Baada ya waraka huo, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Nay ili kumsikia anazungumziaje hilo ambapo alisema hawezi kuzungumza juu ya suala hilo.

“Siwezi kuzungumzia chochote kuhusiana na hilo,” alisema Nay.

Mbali na Skaina, wiki kadhaa zilizopita msanii wa Bongo Fleva, Faidha Omary ‘Sister Fay’ naye aliibuka na kudai kuzaa na Nay huku akisema kwamba amemtelekeza, lakini alipoulizwa Nay mwenyewe alikataa katakata kwamba mtoto huyo siyo wake.

MTAALAM WA SAIKOLOJIA

Akizungumza na gazeti hili juu ya tabia iliyoshamiri ya baadhi ya wanaume kutelekeza watoto na mama zao, Mtaalam wa Saikolojia ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Chris Mauki ambaye ni mbobezi katika elimu ya saikolojia alisema kuwa, jambo hilo linachangiwa na mambo mengi.

“Inaitwa child neglect ambayo inafanywa zaidi na akina baba lakini zipo pia kesi za akina mama ambao wametelekeza watoto.

“Kwanza siku hizi mapenzi yanakufa mapema hivyo mwanaume anaamua kuingia mitini. Tamaa ya kuolewa imewaponza akina dada wengi na kujikuta wakiishia kuzalishwa na kuachiwa majukumu ya kulea.

“Kiukweli hofu na utu vimepungua sana, watu wamekuwa hawajali kupoteza au kutelekeza damu zao.

“Cha kufanya ni wahusika kuongeza umakini katika kuchagua wenza wa kuwa nao na kuwa waaminifu. Ni wakati mwafaka kwa wale waliotelekeza watoto wao kurudisha ule utu wa awali na kuanza sasa kuwahudumia watoto wao na Mungu atawabariki,” alisema Dk. Mauki.

Source: Udaku