Mwanzilishi Wa Neno Bongo Fleva Asema.

Mtangazaji mkongwe wa redio, Mike Mhagama, amesimulia jinsi alivyolianzisha jina ‘Bongo Flava.’ Kupitia podcast yake mpya ‘Maktaba ya Bongo Flava’ itokayo kila siku za Alhamis, amesema kipindi hicho alikuwa anaendesha kipindi cha DJ Show cha Radio One akishirikiana na Sebastian Maganga.

Amesema kipindi hicho walikuwa wakicheza zaidi nyimbo za nje lakini walikuja kuamua kutenga dakika 30 za kucheza aina fulani ya muziki ukiwemo wa nyumbani.

“Ilipofika dakika 30 za muziki wa R&B siku hiyo nilikuwa kwenye usukani na kwa mbwembwe nilicheza nyimbo ya kundi la R&B lililoitwa Four Crews Flavour na baadaye kuiunganisha na wanadada wakali kabisa wakati huo wakiitwa Unique Sisters,” anasimulia Mike.

“Kwa vile midundo, mpangilio, lugha na utaalam wa muziki wenyewe kamwe huwezi kufananisha na ule wa Soul 4 Real kwa mfano au Sisters With Voices kutoka Marekani, lakini tulipenda kutofautisha kati ya aina hizi mbili za muziki na ndipo session hii niliibatiza jina ambayo ingetofautisha R&B ya Marekani na ile ya kwetu. Niiipa session hii jina la ‘Bongo Flava,’ hii ilikuwa mwaka 1996,” ameongeza.

“Na ndio ulikuwa mwanzo wa neno Bongo Flava, likiwa na maana ya muziki wenye mahadhi ya nje lakini wenye vionjo na ladha ya Tanzania na si vinginevyo. Lengo langu kuu kuupa muziki huu jina hili ni kuutofautisha na muziki ule wa Marekani.”

Kwenye kipindi hiki pia Mhagama ameeleza jinsi mwaka 2007 alivyozima ubishi wa baadhi ya watu waliokuwa wakijinadi kuwa ndio walianzisha neno Bongo Flava. Anasema watu hao walialikwa na Clouds FM kwenda kuelezea hoja yao mbele yake lakini waliingia mitini.

Source: Dizzim Online