James Dandu ‘Mtoto wa Dandu’ siyo jina geni katika masikio ya mfuatiliaji wa Bongo Fleva lakini wangapi wanamkumbuka au hata kuutambua mchango wake katika Muziki wa Kizazi Kipya Tanzania?
James Dandu au kwa jina
lingine Cool James Massive; ‘CJ Massive ‘ alizaliwa Julai 5, 1970, Mwanza
nchini Tanzania.
Alisoma shule ya Msingi Kurasini na baada ya hapo, yeye, mama yake na ndugu
zake walihamia jijini Stockholm,
Sweden
alikoishi kwa kipindi kirefu. ‘Mtoto wa Dandu’ alianza kuimba wakati mdogo kanisani. James Dandu aliingia rasmi kwenye sanaa ya muziki
mwaka 1988 kitaaluma zaidi, alianza mwaka
1983 jijini Stockholm ambapo
alitoa singo kadhaa zikiwa katika staili ya Euro-House. Mwaka 1992 aliachia
albamu yake ya kwanza ambayo hata hivyo haikupata mafanikio makubwa. Mwaka 1993
, aliungana na msanii mwingine kutoka Afrika Mashariki, Andrew Muturi na kuunda
kundi lililokwenda kwa jina la “SwahiliNation”. Wasanii wengine
wawili wakajiunga kwenye kundi hilo.
Baadaye, James Dandu alijitoa kwenye kundi hilo na kuungana na Mkongomani, Jose
Masena ‘Black Teacher’ na kutoa albamu mbili zilizowatambulisha vyema sehemu
mbalimbali; Undercover Lover (1992) na Zooming You (1995 ) iliyokuwa na wimbo
ulioitwa “Dr . Feel Good” Wakapata mafanikio makubwa na kuingiza pesa ya maana.
Kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata akiwa na mwenzake, Black Teacher , Mtoto wa Dandu aliamua kurudisha majeshi nyumbani kwa lengo la kuja kuibua na kuinua vipaji Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Baada ya Mtoto wa Dandu James kutembelea nyumbani Afrika mwaka 1994 alikuwa na msukumo mkubwa kuiwakilisha Tanzania baada ya kuhudhuria tamasha Kenya ambapo kwa wakati huo Koffi Olomide alikuwa anatumbuiza akasema “Niligundua katika show yake kwamba mashabiki walifurahia ladha za kiafrika licha ya Koffi kuimba kwa lugha ya Lingala. Aliporudi Tanzania alikuja na staili mpya ya uimbaji wa nyimbo za taratibu ( R & B ) ambao haukuwa umezoeleka sana kwa kipindi hicho. Akajipatia umaarufu mkubwa ndani ya kipindi kifupi. Hakuishia hapo, aliendelea kuingiza ubunifu katika kazi zake akawa anachanganya R &B ya kisasa, Rhumba na Ndombolo (staili iliyokuwa maarufu sana nchini Zaire kipindi hicho). Akatoa albamu nyingine kama Soft Like a Pillow(1997) , Bi Harusi (1998) na Sukuma Land (2002).
Miongoni mwa ngoma ambazo mpaka leo zikipigwa lazima watu watulie ni “Sina Makosa” ambayo aliurudia wimbo wenye jina hilohilo uliopigwa na Les Wanyika kutoka Kenya. Ngoma hii ilimtambulisha sanaAfrika Mashariki yote hususan nchini Kenya. Mtoto wa Dandu aliiongezea ala za kisasa za hip-hop na kujipatia umaarufu mkubwa sio tu Afrika Mashariki, lakini katika sehemu nyingine za ulimwengu. Wimbo ulipanda chati katika bara la Ulaya na marekani. Wimbo huo ulipatikana katika Milenia ya Afrika ya mwaka 1999, albamu ya tisa ya Cool James aka Mtoto wa Dandu. Lakini muziki wa Kiafrika ulikuwa eneo jipya la Cool James. Ingawa alikuwa msanii aliyeanza na kufanya vizuri nchini Sweden akirekodi na kuuza albamu tangu 1986, hakuwa na nafasi wala uzoefu kuhusu kufanya muziki kwa soko la Afrika.
Pia alifanya remix ya wimbo wa Mamu akiwa na mkali Madilu System ambao ama kwa
hakika ulibamba sana kwenye chati
Mwaka 1999, James Dandu aliamua kuanzisha tuzo alizoziita “Tanzania
Music Awards” ambazo hivi sasa zinajulikana kama
Kili Music Awards baada ya kuanza kudhaminiwa na bia ya
Kilimanjaro. James Dandu ndiye aliyefanikisha usajili wa tuzo hizo kwa
kushirikiana na Basata chini ya Wizara ya Elimu na Utamaduni zama hizo
Habari za kifo cha mwimbaji na
msanii wa kiTanzania alieishi Sweden, Cool James aka Mtoto wa Dandu, ilikuwa ni
pigo kubwa kwa tasnia ya Muziki wa Kizazi Kipya Afrika Mashariki. Mtoto wa
Dandu ambaye alikuwa na umri wa miaka 30, alifariki katika ajali ya gari Agosti 27 mwaka 2002, kwa ajali ya gari iliyotokea eneo
la Makumbusho jijini Dar es Salaam, nyota yake ikiwa inang’ara bado na kuzua
simanzi kubwa miongoni mwa mashabiki zake. Mtoto
wa Dandu alizikwa nyumbani
kwao Mwanza.
Kabla ya Kufariki, alikuwa bado hajamaliza kurekodi kazi zake mpya katika
Studio ya Master Jay pale MJ RECORDS. Aliacha watoto wawili Caroline JJ na Michael wakiwa bado wadogo pamoja na mjane, Devota Chuwa.
Hadi leo, anajulikana zaidi kwa kutumia
vionjo vya wimbo wa Lingala “Sina Makosa” kutoka maktaba ambapo Les Wanyika
waliwahi kutamba nao.
Cool James alikuwa mfanyabiashara ambaye aliamini katika kuchanganya ujuzi na akili nzuri ya biashara katika muziki na James aliamua kwamba yeye alitaka aina hiyo ya mwamko katika matamasha yake kwa ladha za afrika pia. Aliandikisha kampuni nyingine ndogo ndani ya kampuni yake
“Dandu Entertainment” kutafuta, kuzalisha na kusimamia wasanii wenye vipaji, walio na utayari wa kujitoa kuitetea sanaa ya Muziki Tanzania.
Cool James aliwahi kusema katika
mahojiano ya radio akizungumzia juu ya albamu yake kabla ya kutolewa akasema ”Watayarishaji Tanzania walikuwa na hofu ya
kuwekeza fedha zao katika mradi mpya. Ninatafuta wasanii wa afrika mashariki na
kuunganisha nyimbo zao zote kwenye albamu moja na hakika Hawa wasanii wa Kenya,
Uganda na Watanzania watapata malipo ya mirabaha kutokana na muziki wao
kuchezwa katika vyombo mbali mbali duniani“
Ni miaka mingi sasa imepita tangu Mtoto wa Dandu aliporejea kwenye makazi yake ya milele. Swali ambalo mimi na wewe tunapaswa kujiuliza: Je, anapewa heshima anayostahili hata kama alishatangulia mbele za haki? Familia yake wakiwemo wanae Caroline -Jamie ‘Malaika ‘ aliyezaliwa mwaka 1994 na Michael James Junior aliyezaliwa 1997 wananufaika na matunda ya kazi za baba yao?