“Mama yangu alikuwa tayari kunipa hela nifanye muziki nilipokata tamaa” – Timbulo

Kupitia XXL ya Clouds FM April 21, 2017 staa wa Bongo fleva Timbulo amesema baada ya kujaribu kwa muda mrefu bila mafanikio alikata tamaa kufanya muziki kwa sababu haukuwa unamlipa na kuhisi anachelewa.

Kutokana hali hiyo alishindwa kulipa pango ya nyumba hivyo kuhama DSM kurudi kijijini ambako mama yake alimsihi arudi mjini akiahidi kumpa hela ili arudi kuendelea na muziki.

“Kuna wakati niliwahi kukata tamaa, nikaona nifanye kazi nyingine tu, lakini watu waliokuwa karibu na mimi walinipa moyo.

“Nilipata usugu sana wakati nafanya muziki kuanzia 2005 mpaka 2010, nikaamua kuacha na kurudi kijijini kwetu kwa sababu ya kushindwa kulipa pango ya miezi miwili ambayo ilikuwa 30,000, 15,000 kila mwezi.

“Niliporudi nyumbani kwetu kijijini Mbeya, mama yangu alinambia kwa nini leo umekata tamaa we mtoto wa kiume hautakiwi kukata tamaa. Akaniambia kuwa yupo tayari kuuza hata mazao na ng’ombe ili nirudi mjini kufanya muziki nitoke, ila nilikataa kuuza mazao ya mama yangu.” – Timbulo.

Source:Millard ayo