Mstari unaotenganisha ‘penzi na urafiki’ ni laini zaidi ya uzi wa buibui, hivyo unahitaji heshima ya hali ya juu, uaminifu wa dhati na utulivu halisi ili usikatike na kuleta maafa ndani ya nyoyo za wahusika.
Kama utairudia vizuri aya hapo juu na kutafakari, unaweza kutumia lugha hiyo ya picha kuunganisha kile ulichowahi kusikia ama kushuhudia pale marafiki tena waliotoka mbali, wanapofikia hatua ya kugeuka kuwa maadui wakubwa kutokana na kusalitiana na kuibiana penzi.
Leo nitawalenga zaidi marafiki wa kiume dhidi ya mrembo wa mmoja kati yao.
“Wanavunja urafiki kwa uzuri wa shemeji zao,” huo ni msemo uliozoeleka unaoonesha madhara ya usaliti wa aina hiyo.
Lakini, wapo marafiki ambao wamefikia hatua ya kuuana kwa visu, kuendeana kwa ‘Kalumanzila’ au hata wenye roho nyepesi kujinyonga kwa hofu ya kuondoa aibu mbele ya dunia.
Kutokana na usaliti huo uliokubuhu, ni dhahiri kuwa wapo pia baadhi ya watu hata wamefikia hatua ya kulea watoto wanaodhani kuwa ni wa kwao na kumbe ni watoto wa rafiki zao wa karibu sana na wanaowaamini. Hiyo ni kwa upande wa wanaume.
Chanzo cha tatizo hilo kubwa la usaliti wa penzi, kwa hakika ni tamaa iliyofungwa kwenye kifurushi cha ukosefu wa heshima, haya, na ukosefu wa hofu ya Mungu kati ya wawili wanaokubaliana kuupasua moyo wa mtu wa tatu anayewaunganisha kama ‘Mashemeji’.
Chanzo kingine ni visasi kutokana na maudhi ambayo huenda yasiendane kabisa na mapenzi. Kwa mfano, mtu anaweza kuamua kufanya usaliti huu kutaka kumkomesha rafiki aliyemdhulumu au aliyemchonganisha na mtu fulani.
Lakini wengine, ni hulka ama uhamasishaji usio wa moja kwa moja kwenye jamii fulani kama uwepo wa misemo maarufu inayotukuzwa katika baadhi ya maeneo kuwa ‘hainaga ushemeji’. Hivyo, wasaliti wanachukulia kama kutembea na shemeji ni jambo la kawaida tu!
Hata hivyo, kwakuwa hata ajali ingawa haina kinga huwa na tabia ama dalili zinazoweza kutajwa, ndivyo ambavyo tabia ama alama za uwezekano wa rafiki kumgeukia mpenzi wako zinaweza kubainika.
Kwanza, baadhi ya marafiki wasio waaminifu, hutumia nafasi ya malalamiko wanayopewa na shemeji zao kuhusu rafiki husika, kuanza kujipenyeza na kuonesha jinsi ambavyo wao ni wema zaidi.
Pili, kwakuwa marafiki hao wasio waaminifu huwa na nafasi ya kusikiliza pande zote mbili, hujikuta wakiyajua vizuri mapungufu ya pande zote mbili na kuanza kampeni chafu inayoongozwa na tamaa, kuanza kuonesha namna wanavyoweza kuziba pengo la udhaifu husika.
Tatu, rafiki mnafiki na mwenye tamaa, huanza kutafuta namna ya kuanza kufanya mawasiliano na shemeji anayemtamani, mawasiliano ambayo yanaweza kuwa hayatiliwi shaka hata kidogo na rafiki husika, lakini yana sumu kali zaidi ya joka ‘cobra’. Lakini kadiri siku sinavyoenda, kwa kutegemea mwitiko wa upande wa pili, hujikuta mawasiliano husika yanaanza kuwa na usiri yakibeba nia ovu.
Kwakuwa rafiki huyo mnafiki anajua mbivu na mbichi kati ya wawili hao, hutumia uongo unaofanana na ukweli uliopitiliza kulaghai na kuidhinisha dhambi yake ya usaliti bila kujali hatari kubwa ya mauaji ya ‘moyo’ wa urafiki inayomkabili, kisa starehe ya muda mfupi.
Kwa upande mwingine wa shilingi, usaliti huo husababishwa kwa makusudi na mwanamke ambaye anaweza kuwa na tabia za kumshusha mpenzi wake mbele ya rafiki zake (rafiki wa mwanaume).
Mwanamke huyo anaweza kuzungumzia udhaifu wa mpenzi wake mbele ya rafiki aliyetambulishwa kwake, kuvaa mavazi au mikao inayoonesha ‘mitego’ kwa shemeji zake na kuomba ‘ofa’ kwa shemeji zake pasipo kumhusisha mpenzi au mmewe.
Hivyo, hupelekea watu wenye tamaa na macho ya ‘kiokote’ kuanza kampeni za kumshawishi kwani huamini ni mtu rahisi wa kutumika kutokana na tamaa iliyomjaa.
Kwa upande mwingine, mwanamke asiye mwaminifu huchukua maamuzi hayo kama sehemu ya kulipa kisasi kwa mpenzi wake akiamini kuwa kwa kutembea na rafiki wa mpenzi wake atakuwa amemuumiza kwa kadiri iwezekanavyo mpenzi wake.
Hata hivyo, kwakuwa Mungu huichukia na kujibu kwa nguvu zote dhambi ya usaliti, wawili hao hawaishi bila kuumbuka hata kama ni mabingwa wa kuficha siri. Na hapo ndipo dhambi ya usaliti huo hugeuka machungu ya kudumu maishani na majuto kwa wahusika.
Kwa mantiki hiyo, ingawa usaliti na uaminifu ni suala linalotoka ndani ya moyo wa mhusika, unapaswa kuchora mstari wa maana kati ya rafiki zako na mpenzi wako.
Hakikisha habari za marafiki zako muwapo kwenye maeneo yenu hazigeuki kuwa habari za kumsimulia mpenzi wako kila kukicha. Mpe habari zako, zenu au mipango ya kupiga hatua.
Tengeneza urafiki wa heshima kati yao na siku zote hakikisha unakuwa mwaminifu pia ili dhambi nzito ya usaliti wao dhidi yako isiwe na uhusiano wowote wa kusababishwa na wewe.
Usimgeuze rafiki kuwa adui mkubwa wa kudumu kwa tama za mwili zitakazoisha ndani ya muda mfupi.
Source: Udaku