ASHA BARAKA: NIPO TAYARI KUMWAGA MPUNGA WA KUTOSHA KUINUA MUZIKI WA DANSI

asha

Mkurungezi wa Kampuni ya ASET na mmiliki wa bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’, Asha Baraka amesema amedhamiria kuuinua tena muziki wa dansi nchini na kwa kuanza ametangaza kutoa pesa taslimu shilingi milioni moja na nusu kila baada ya miezi mitatu kwa waandishi wa habari za burudani ambao wataandika habari nyingi pamoja na makala kuhusu muziki wa dansi nchini.

Mmiliki wa bendi hiyo amesema hayo alipozungumza na Global Digital:

“Vyombo vya habari hasa hasa magazeti na tovuti zimekuwa zikiandikwa habari chache za muziki wa bendi licha ya kuwa na matukio mengi, sasa nimekaa nikaona nianzishe mashindano ya kuandika habari na makala nyingi za muziki wa dansi, mshindi wa kwanza kwa upande wa magazeti atapata milioni moja, wa pili na wa tatu atapata laki mbili kila mmoja halafu kwa upande wa tovuti tutatoa laki tano. Ili mtu kuwa mshindi unatakiwa kuandika story nyingi pamoja na makala kuhusu muziki wa bendi, bendi yoyote siyo lazima Twanga Pepeta.

Halafu ukishaandika na stori ikatoka utaleta nakala za gazeti pale ofisini kwetu au link za tovuti, unaweza kuleta kazi zako za mwezi mzima alafu mwezi wa kumi na mbili tutakaa jopo la wachambuzi na kuangalia nani ni mshindi. Shindano limeanza tarehe moja mwezi huu kwa hiyo kila baada ya miezi mitatu tutawatoa washindi na zawadi zao watapewa.”

Mwanamama huyo nguli wa muziki wa dansi nchini pia amesisitiza kwamba mshindi huyo atakapopatikana ataandaliwa sherehe maalum pamoja na kumtunza ambapo bendi mbalimbali zitapiga dansi live kwa ajili ya mshindi, Asha amewaomba waandishi wengi nchini kuchangamkia fursa hiyo.

Habari imeandikwa na @Joplus_

Source: Global Publishers