YANGA jana iliongeza utamu kwenye mbio za ubingwa baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanaipandisha Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa uwiano mzuri wa mabao ikiwa na pointi 62 sawa na Simba iliyo nafasi ya pili. Yanga sasa inakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kutetea taji lake la ubingwa kwani pointi saba zinahitajika kutangaza ubingwa. Mabingwa hao watetezi wamebakiwa na mechi tatu na Simba imebakiwa na mechi mbili, jambo ambalo linawafanya wekundu hao wa Msimbazi kukomaa kushinda mechi hizo huku ikikazana kufanya maombi Yanga ifanye vibaya katika mechi zilizosalia, ikiwa vinginevyo itashuhudia ubingwa ukienda kwa wapinzani na wenyewe wakiukosa kwa takriban mwaka wa tano sasa.
Simon Msuva aliiandikia Yanga bao la kuongoza katika dakika ya 39 kwa kichwa baada ya kuunganisha mpira wa kona uliopigwa na Geofrey Mwashiuya. Dakika ya 45, Kagera ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Mbaraka Yusuf aliyeachia shuti kali lililomzidi kipa wa Yanga, Benno Kakolanya. Hata hivyo, mchezaji huyo hakumaliza mechi baada ya kutolewa dakika ya 88 kwa kadi nyekundu na mwamuzi Ngole Mwangole wa Mbeya baada ya kumfanyia madhambi Kelvin Yondani.
Yanga iliandika bao la pili katika dakika ya 52 likifungwa na mchezaji wake, Obrey Chirwa, aliyeunganisha pasi ya kiungo Haruna Niyonzima, kabla hajaujaza mpira katika nyavu zilizokuwa zikilindwa na kipa wa zamani wa timu hiyo Juma Kaseja. Katika mechi hiyo timu hizo zilicheza soka ya kawaida, lakini ni Yanga ndio walionekana kucheza kwa kujipanga zaidi huku wachezaji wake wakikosa mabao mara kadhaa ikiwemo dakika ya 48 pale Amis Tambwe aliposhindwa kufunga akiwa peke yake na kipa Kaseja.
Msuva alikosa tena bao katika dakika ya 57 ambapo akiwa kwenye nafasi nzuri alipiga mpira pembeni. Yanga: Benno Kakolanya, Hassan Kessy/Juma Abdul, Mwinyi Hajji Ngwali, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Obrey Chirwa/Matheo Anthony, Geoffrey Mwashiuya/Geoffrey Mwashiuya. Kagera Sugar: Juma Kaseja, Godfrey Taita/Themi Felix, Mwaita Gereza, Babu Ali Seif/Anthony Matogolo, Mohammed Fakhi, George Kavilla, Suleiman Mangoma, Ally Nassor, Mbaraka Yusuf, Ame Ally, Edward Christopher/Japhet Makalao.