Serengeti Boys watoa pole kwa watanzania

KOCHA Mkuu wa Serengeti Boys Bakari Shime, ametuma salamu za rambirambi kwa Watanzania wote kufuatia vifo vya wanafunzi wa shule ya Lucky Vincent, Arusha.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Shime alisema anatoa pole kwa niaba ya benchi la ufundi na wachezaji wote na kusema Tanzania imepoteza kizazi ambacho baadhi yao wangeweza kuwa wachezaji.

“Nitoe pole kwa Watanzania wote kwa niaba ya Serengeti Boys, tumeguswa na tukio la ajali lililotokea kule Karatu, Arusha,” “Taarifa hii ni ya huzuni sana lakini Mungu ndiye amepanga, kwa niaba ya benchi la ufundi na wachezaji wote wa Serengeti Boys natoa pole kwa Rais John Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, familia, ndugu jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu,” alisema Shime.

Pia Shime alisema jana walianza mazoezi mepesi baada ya juzi kufika salama Gabon kwa ajili ya maandalizi ya mchezo ya kwanza Jumatatu dhidi ya Mali. Mei 6, 2017 basi dogo lililokuwa limebeba wanafunzi lilipata ajali kwenye mlima wa Rhotia, Karatu, Arusha ambalo lilikuwa limebeba wanafunzi waliokuwa wanakwenda kwenye mtihani wa ujirani mwema katika shule ya msingi Karatu ambapo wanafunzi 33, walimu wawili na dereva walikufa. Jana Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan aliongoza wananchi kuaga miili ya waliofariki katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.