SALA YA JENEZA

SALA YA JENEZA

Haki ya maiti Mwislamu baada ya kumuosha, kumvika sanda, na kabla ya kumzika ni kumsalia. Na Sala ya kumsalia maiti Mwislamu hujulikana kwa SALA YA JENEZA na ni FARADHI KIFAYA (yaani ni kitendo ambacho wakikifanya baadhi wengine husamehewa) na kisipofanywa kabisa basi Waislamu wote wa sehemu ile hupata dhambi. Alikuwa Mtume S.A.W. akiwasalia maiti wa Kiislamu na ingawa yeye wakati mwingine akitokea mtu kafa na deni alikuwa hamsalii lakini hata hivyo alikuwa akiamrisha Masahaba zake wamsalie. Mtume S.A.W. kasema katika Hadithi iliyotolewa na Nnasaai, “

“صَلُّوا عَلَى صَاحِبِكُمْ فَإِنَّ عَلَيْهِ دَيْنًا.”

Maana yake, “Msalieni rafiki yenu kwa hakika ana deni.”

MASHARTI YA SALA YA JENEZA.
Masharti ya Sala ya jeneza ni sawasawa na masharti ya Sala zote za kawaida kama vile: Tohara ya uchafu na janaba, kuusitiri utupu (uchi), kuelekea kibla na kadhalika. Lakini Sala ya jeneza huwa haina wakati maalum isipokuwa zile nyakati tatu zilizoharamishwa kusaliwa Sala. Kama alivyoiita Mtume S.A.W. Sala ya jeneza ni Sala katika Hadithi iliyotolewa na Nnasaai, Mtume S.A.W. aliwaamrisha Masahaba zake, “

“صَلُّوا عَلَى صَاحِبِكُمْ.”

Maana yake, “Msalieni rafiki yenu.”

FARIDHA ZA SALA YA JENEZA.
Sala ya jeneza hufaridhisha (hulazimisha) yafuatayo: Kusimama katika Sala, nia, kusoma Suratil Faatiha (Al-Hamdu), kumshukuru Mwenyezi Mungu, salamu juu ya Mtume S.A.W., takbira 4, dua na kutoa salamu.

Ziko Hadithi nyingi zinazothibitisha kauli hizi. Katika Hadithi iliyopokelewa na Jaabir bin Abdallah R.A.A. na iliyotolewa na L-Bukhari, kasema “Mtume S.A.W. alimsalia Nnajaashiyi mfalme wa Habasha wakati alipofariki kwa takbira 4, “
“أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ صَلَّى عَلَى النَّجَاشِيِّ فَكَبَّرَ أَرْبَعًا’.”

Maana yake, “Hakika Mtume S.A.W. alimsalia Nnajaashiyi akatoa takbira nne.”
Pia Hadithi iliyopokelewa na Talha R.A.A. kasema “Kuna siku nilisali nyuma ya Sahaba Ibn Abbas R.A.A. Sala ya jeneza akasoma Suratil Al-Hamdu, kasema,

“فَقَرَأَ بِفَاتِحَةِ الْكِتَابِ قَالَ: لِيَعْلَمُوا أَنَّهَا سُنَّةٌ.”

Maana yake, “Akasoma Fatihatil Kitaaba kasema: Ili waijue kwamba ni Sunna.”

NAMNA INAVYOSALIWA SALA YA JENEZA.
Namna ya kusali Sala ya jeneza ni kama ifuatavyo.

a) Jeneza litawekwa chini kuelekea kibla.

Inapendeza Imamu atakayetangulia mbele kusalisha Sala ya jeneza awe Mwislamu mchaMungu mwenye kuhifadhi Qurani na kufahamu na kufuata Sunna za Mtume S.A.W.. Kama alivyotuelezea Mtume S.A.W. katika Hadithi iliyotolewa na Rabi`i, “

“أوْلىَ بالصَّلاَةِ عَلىَ المَيِّتِ أفْضَلُ القَوْمُ وَرِعًا ، وَأسَنُّهُمْ فِيْ ذِكْرِ اللهِ.”

Maana yake, “Wa kwanza wa kumsalia maiti ni wachaMungu na wenye kumdhukuru sana Mwenyezi Mungu.”

c) Imamu atasimama mbele ya maiti; ikiwa maiti yule ni ya mwanamume Mwislamu basi Imamu atasimama upande wa kichwani mwa yule maiti, na ikiwa maiti yule ni ya mwanamke Mwislamu basi Imamu atasimama upande wa kifuani mwa yule maiti. Na Waislamu watasimama katika safu ya nyuma ya Imamu ambao wanajulikana kama ni maamuma. Na inapendeza kwa ajili ya maiti kukubaliwa dua, safu za wale Waislamu wanaomsalia zisiwe chini ya safu tatu. Kama alivyotufahamisha Mtume wetu S.A.W. katika Hadithi iliyotolewa na Abu Daud, “

“مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَمُوتُ فَيُصَلِّي عَلَيْهِ ثَلاثَةُ صُفُوفٍ مِنَ الْمُسْلِمِينَ إِلاَّ أَوْجَبَ.”

Maana yake, “Hakuna Mwislamu anayekufa wakamsalia safu tatu za Waislamu ila anakubaliwa.”

d) Kisha Imamu ataweka nia moyoni mwake kwamba anamsalia maiti. Na maamuma watafanya hivyo hivyo.

e) Tena atakabbir atasema “ALLAAHU AKBAR,” na baada ya takbiir atasoma SURATIL FAATIHA kwa siri. Na maamuma watafanya hivyo hivyo.

f) Atakabir takbiira ya pili na atasoma SURATIL FAATIHA kwa siri. Na maamuma watafanya hivyo hivyo.

g) Atakabbir takbiira ya tatu ATAMSHUKURU MWENYEZI MUNGU na kumsalia MTUME S.A.W. na ataomba ASAMEHEWE DHAMBI ZAKE NA WAUMINI WANAUME NA WAUMINI WANAWAKE. Baada ya hapo ATAOMBA DUA kama zilivyotajwa hapo chini.

h) Na baada ya kusoma dua ATAKABBIR takbiira ya nne atatoa salamu inayosikika na maamuma tu na ndio mwisho wa Sala.

ALIYEPITWA NA SALA YA JENEZA.
Sala ya jeneza haina masharti ya kulipa kama ilivyo Sala ya Faridha. Kwa hali hiyo Mwislamu anayemsalia maiti akapitwa na baadhi ya Sala ya jeneza kama vile Takbiir au Suratil Hamdu si lazima kurudia bali inatosha aliyowahia katika Sala ya jeneza.

DUA YA KUMUOMBEA MAITI.
Imekuja katika riwaya za Mtume S.A.W. dua nyingi za Sala ya jeneza. Hapa nitaziandika baadhi yake tu. Na mahali pa kusomwa dua ni baada ya takbiira ya tatu ya Sala ya jeneza. Dua ya kwanza katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na iliyotolewa na Ibn Maajah, “

“اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِحَيِّنَا وَمَيِّتِنَا وَشَاهِدِنَا وَغَائِبِنَا وَصَغِيرِنَا وَكَبِيرِنَا وَذَكَرِنَا وَأُنْثَانَا ، اللَّهُمَّ مَنْ أَحْيَيْتَهُ مِنَّا فَأَحْيِهِ عَلَى الإِسْلامِ وَمَنْ تَوَفَّيْتَهُ مِنَّا فَتَوَفَّهُ عَلَى الإِيمَانِ ، اللَّهُمَّ لا تَحْرِمْنَا أَجْرَهُ وَلا تُضِلَّنَا بَعْدَهُ.”

ALLAAHUMMA GHFIR LIHAYYINAA WAMAYYITINAA WASHAAHIDINAA WAGHAAIBINAA WASAGHIIRINAA WAKABIIRINAA WADHAKARINAA WAUNTHAANAA. ALLAAHUMMA MAN AHYAYTAHU MINNAA FA-AHYIHI `ALAL ISLAAMI WAMAN TAWAFFAITAHU MINNAA FATAWAFFAHU `ALAL IMAANI. ALLAHUMMA LA TAHRIMNAA AJRAHU WALA TUDHILLANAA BA`ADAHU.

Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu! Samehe (dhambi) za walio hai wetu na maiti zetu na mashahidi wetu na wasiohudhuria kwetu na wadogo wetu na wakubwa wetu na wanaume wetu na wanawake wetu. Ewe Mwenyezi Mungu! Unayemhuisha kati yetu basi mhuishe katika Uislamu na unayemfisha kati yetu basi mfishe katika imani. Ewe Mwenyezi Mungu! Usitunyime ujira wake na wala usitupoteze baada yake.”

Pia dua nyingine katika Hadithi iliyopokelewa na Jubair bin Nufair R.A.A. anasema kwamba alimsikia `Auf bin Maalik R.A.A. akisema “Mtume S.A.W. alisali Sala ya jeneza nikaihifadhi dua yake alisema, “

‘‘اللَّهُمَّ اغْفِرْ لَهُ وَارْحَمْهُ ، وَعَافِهِ وَاعْفُ عَنْهُ وَأَكْرِمْ نُزُلَهُ وَوَسِّعْ مُدْخَلَهُ وَاغْسِلْهُ بِالْمَاءِ وَالثَّلْجِ وَالْبَرَدِ وَنَقِّهِ مِنَ الْخَطَايَا كَمَا نَقَّيْتَ الثَّوْبَ الأَبْيَضَ مِنَ الدَّنَسِ ، وَأَبْدِلْهُ دَارًا خَيْرًا مِنْ دَارِهِ وَأَهْلا خَيْرًا مِنْ أَهْلِهِ وَزَوْجًا خَيْرًا مِنْ زَوْجِهِ وَأَدْخِلْهُ الْجَنَّةَ وَأَعِذْهُ مِنْ عَذَابِ الْقَبْرِ أَوْ مِنْ عَذَابِ النَّارِ’’

ALLAAHUMMA GHFIR LAHU WARHAMHU WA`AAFIHI WA`AFU `ANHU WA AKRIM NUZULAHU WAWASSI`I MUDKHALAHU WAGHSILHU BILMAAI WATHILJI WALBARADI WANAQQIHI MINAL KHATAAYAA KAMAA NAQQAYTA TH-THAUBAL ABYADHA MINAL DDANAS. WA ABDILHU DAARAN KHAIRAN MIN DAARIHI WA AHLAN KHAIRAN MIN AHLIHI WAZAUJAN KHAIRAN MIN ZAUJIHI WA ADKHILHU JANNAATI WA A`IDH-HU MIN `ADHAABIL QABRI AU MIN `ADHAABI NNAAR.

Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu! Msamehe na umrehemu, na umhurumie. Na umpokee kwa heshima na ulipanue kaburi lake, na muoshe kwa maji na barafu na baridi na msafishe madhambi kama inavyosafishwa nguo nyeupe iliyopata uchafu.
Na mbadilishie makaazi yaliyo bora kuliko makaazi aliyokuwa nayo, na familia bora kuliko familia yake, na mke alie bora kuliko mkewe na muingize Peponi na mkinge na muepushe na adhabu ya kaburini na adhabu ya Motoni.” `Auf akazidi kusema “Nilitamani huyo maiti anayeombewa niwe ndio mimi.”

Na dua ya tatu ni hii ifuatayo, “

“يَبْعَثُ مَنْ فِي الْقُبُورِ . هُوَ الأَوَّلُ وَالآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ . رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَحْمَةً وَعِلْمًا فَاغْفِرْ لِلَّذِينَ تَابُوا وَاتَّبَعُوا سَبِيلَكَ وَقِهِمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ* رَبَّنَا وَأَدْخِلْهُمْ جَنَّاتِ عَدْنٍ الَّتِي وَعَدْتَهُم وَمَنْ صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ إِنَّكَ أَنْتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ * وَقِهِمْ السَّيِّئَاتِ وَمَنْ تَقِي السَّيِّئَاتِ يَوْمَئِذٍ فَقَدْ رَحِمْتَهُ وَذَلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ”.

story@moodyhamza