MAFANIKIO YA MAISHA YAKO YANATEGEMEA TABIA YAKO.

2

Tafiti ambazo zimewahi kufanywa na wanasoikolojia mbalimbali kuhusu maisha ya mwanadamu na mazingira yake hususani suala zima la mafanikio, zilitoa majibu ya kwamba maisha ya mwanadamu yanaathiriwa kwa kiwango kikubwa na vitu vikubwa viwili ambavyo ni;

Jambo la kwanza ni kuishi kwa kukariri.
Suala hili ndilo ambalo limekuwa limeathiri maisha ya wengi kwa asilimia kubwa sana. Watu wanashindwa kuishi kulingana na jinsi ambavyo dunia inakwenda kasi.

Hebu tunawatazame wafanyabiashara wangapi ambao leo hii ambao walianza kufanya biashara tangu muda mrefu kabla ya kukua kwa teknolojia hususani masuala ya mitandao ya kijamii ambao leo hii wanatumia mitandao hiyo ya kijamii katika kuzitangaza bidhaa au huduma zao?

Kimsingi ukifanya tathimini utagundua ni wachache sana. Unajua ni kwanini wapo wachache? kwa sababu wameshazoea na kuishi maisha ya kukariri huku wakiamini ya kwamba kutumia mitandao ya kijamii ni suala gumu kwao.

Hii ni ishara ya kwamba imani waliyonayo ni ngumu sana ambayo hawawezi kubadilika hata kupelekea wao kutokuamini ya kwamba wanaweza kujitangaza kupitia mitandao ya kijamii. Imani waliyonayo ni kwamba kutumia mitandao ya kijamii ni suala la kupoteza muda.

Lakini ukweli haupo hivyo ndugu yangu mwenye tabia kama hizo, tambua na elewa ya kwamba kuna watu ambao inabidi wakutambue kwa shughuli ambayo unaifanya ambao kimsingi wanaishi mbali na sehemu ulipo.

Ewe mfanyabiashara acha kuishi kimazoea na kuamini ya kwamba mahali ulipo sasa panatosha, ila amini ya kwamba ipo haja leo ya kujua ya kwamba wapo baadhi ya wadau wanapenda kujua hicho ambacho unakifanya.

Jambo la Pili ambalo linaathiri Maisha ya wengi ni kuishi kimazoea.
Kuishi kimazoea ndiko kunakotufanya tuishi kwa manung’uniko na masikitiko hasa katika maisha haya ya kila siku. Hebu tazama kwa mfano utawala huu wa awamu ya tano jinsi ambavyo unafanya kazi kila mmoja kwa nafsi yake moyoni ana yake ya kusema, unajua ni kwanini kwa sababu watu wengi tulikwisha kuzoea kuishi maisha ya kimazoea sana, hivyo tunajikuta kwa asilimia kubwa tunashindwa kuendana na kasi hiyo na tunabaki tunalalamika kwa sababu tulishazoea kuishi kimazoea.

Kuishi kimazoea ni kubaya sana mpenzi msomaji wa makala haya kwa sababu pindi changamoto yeyote ijitokezapo kwetu huwa ni kikwazo kikubwa cha kuweza kulifikia lengo. Leo hii ukimkuta mtu ambaye anafanya jambo fulani na ukamshauri afanye jambo jingine atakataa, unajua ni kwanini atakataa? atakataa kwa sababu amezoea kufanya jambo lake la awali hivyo kubadili kufanya jambo jingine kwake hutengeneza hofu ya kushindwa.

Ndugu yangu ambaye kwa hali yeyote ile unataka kufanikiwa, na si kufanikiwa tu, bali kufanya mafanikio yako yamguse kila mmoja wetu kwa namna moja ama nyingine hakikisha ya kwamba usiishi katika misingi ambayo ni ya kukariri au kuishi katika mtazamo wa kimazoea, kwani kufanya hivi ni kujiua mwenyewe.

Nakusihi tena kwa kukumbusha ujio wako hapa dunia si kwa bahati mbaya ila ni kwa kusudio maalum amini ya kwamba wewe ni zaidi ya matajiri wakubwa waliopo sasa, pia tumia muda mwingi kumshukuru Mungu kwa kukupa hekima na akili ya kuweza kufikiri, pia muombe akupe ujasiri wa kuweza kutenda mambo kwa fikra na mitazamo chanya.

Story by:@Joplus_

Source:Muungwana Blog