KWA NINI UISLAMU UNAHARAMISHA RIBA NA KUHIMIZA SADAKA.

Na tuanze na kuangalia Qur`ani Tukufu inasema nini kuhusu riba. Katika Sura ya Baqarah , Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuonya:

“Ambao wanakula riba, hawainuki, ila kama ainukavyo aliyezugwa na shetani kwa wazimu. Hayo ni kwa sababu wanasema kuwa biashara ni kama riba. Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na ameharamisha riba. Na aliyefikiwa na na mawaidha kutoka kwa Mola wake, akakoma, basi yake ni yaliyokwishapita na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wanaorejea, basi hao ndio watu wa motoni; wao ni wenye kukaa humo milele. Mwenyezi Mungu huipunguza riba na huizidisha sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila kafiri afanyae dhambi.” (2:275-276).

Uharamisho wa Qur`ani Tukufu juu ya riba uko wazi. Katika aya zinazofuata (2:278-279) Mwenyezi Mungu Mtukufu anatangaza kwamba wale wanaojiingiza katika kula riba ni “…basi jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake…..” Pia zipo hadithi nyingi zinazohusu uharamisho wa riba na miongoni mwa hadithi hizo moja inatosha kwa lengo letu. Katika Sahih Muslim, Abu Dawud, na al-Tirmidhi, Jabir ibn Abdullah anasimulia hadithi ifuatayo kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.):

“Mjumbe wa Mwenyezi Mungu Mtukufu (s.a.w.w.) amewalaani wanaopokea riba, wanaofanya biashara ya riba, (wakopeshaji na wakopaji kwa riba), wale wanaoshuhudia mapatano ya riba, na wale wanaosajili biashara za riba. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema, ‘Wote hao ni washiriki.”’

Kwanza tuelewe riba ina maana gani. Katika maana ya kilugha, riba maana yake ni nyongeza au ongezeko la kitu juu na zaidi ya kiwango au idadi yake ya mwanzo. Kwa kawaida hutumika kwa fedha inayokopeshwa kwa mtu fulani na kiasi fulani cha ziada kilipwe juu na zaidi ya kiasi halisi kilichokopeshwa. Dhuluma iliyopo katika mpango kama huu iko wazi; mkopaji ni muhitaji na wakati ambapo kiasi halisi cha mwanzo cha mkopeshaji kinahakikishwa pamoja na kiasi cha nyongeza, haizingatii hali au uwezo wa mkopaji. Hakuna hatari wala shaka kwa mkopeshaji; lakini tatizo lipo kwa mkopaji tu. Qur`ani Tukufu inazungumzia jambo hili kwamba kiasili ni udhalimu.

story@moodyhamza